Marehemu Steven Kanumba |
MAELFU ya wapenzi wa sanaa ya filamu nchini, alfajiri ya kuamkia jana waliduwaa mithili ya watu waliopigwa sindano ya ganzi baada ya kuenea kwa taarifa za kifo cha ghafla cha msanii namba moja wa filamu nchini, Steven Charles Kanumba (28). Taarifa za kifo cha Kanumba zilisambaa kwa kasi mithili ya moto katika nyika kavu na kuikuta alfajiri ya jana, ikigeuka kibarua kigumu kwa idadi kubwa ya watu, kusaka stesheni mbalimbali za redio, televisheni mitandao ya kompyuta huku wengine wakihangaika kupiga simu huku na kule, kutafuta ukweli wa tukio hilo,lililotikisa si Tanzania tu bali ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Kanumba alifariki usiku wa kuamkia jana nyumbani kwake, Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam. Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi, Kanda ya Kinondoni, Charles Kenyela, ziinaeleza kuwa kifo cha msanii huyo kilitokana na ugomvi uliotokea kati yake na mpenzi wake ndani ya nyumba yake. Taarifa za kifo cha Kanumba zilianza kusambaa kuanzia saa 10.00 alfajiri na kuenea kwa kasi ambapo hadi kufikia saa moja asubuhi, mamia ya watu walikuwa wamejazana nyumbani Kanumba kutaka kuthibitisha habari hizo. Kadri muda ulivyozidi kusogea ndivyo idadi ya watu ilizidi kuongezeka nyumbani kwa msaani huyo ambaye amejizolea umaarufu mkubwa kutoka na filamu zake kuuzwa na kuoneshwa katika vituo mbalimbali vya televisheni, ndani na nje ya nchi. Miongoni mwa watu waliomiminika kwa haraka nyumbani kwa kanumba jana ni wasanii wa fani mbalimbali nchini, wanasiasa na viongozi mbalimbali wa Serikali Chanzo cha kifo chake Kwa mujibu wa maelezo ya mdogo wake aitwaye Seth ambaye alikuwepo eneo la tukio, alisema kaka yake alishinda nyumbani na baada ya kula chakula cha jioni, alimwambia wajiandae kutoka.Seth alisema kuwa wakati Kanumba akiwa tayari amejiandaa, walisikia mlio wa gari lifunga breki nje ya nyumba. Alisema gari hilo lilikuwa limemleta mpenzi wa kaka yake msanii wa filamu, Elizabeth Michael maarufu kwa jina la Lulu ambaye aliingia ndani na kwenda moja kwa moja chumbani kwa Kanumba.Baada ya kuingia ndani, muda mfupi alisikia sauti zilizoashiria kuwa kulikuwa na ugomvi kati ya wapenzi hao. “Ghafla ulizuka mzozo ndani na dakika chache baadaye, Lulu alitoka na kuja kuniambia kuwa Kanumba amedondoka baada ya kujigonga ukutani na kwamba yupo taabani hajitambui,” alisema Seth.Alisema alipoingia chumbani, alimkuta kaka yake akiwa katika hali mbaya hivyo akaamua kumpigia simu daktari wake, ambaye alipofika na kuwashauri wampeleke haraka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kupatiwa matibabu. Seth alisema kabla ya kufika Muhimbili walipitia Kituo cha Polisi cha Oysterbay kupatiwa Fomu ya matibabu (PF3). Hata hivyo, baada ya polisi kupata maelezo ya awali ya ugomvi huo, walimshikilia Lulu kituoni hapo na kumwacha Seth akimpeleka Kanumba hospitali. Alisema walipofikia Hospitali ya Muhimbili, madakati waligundua kuwa tayari Kanumba alishaaga dunia. Kamanda Kenyela Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema Kanumba alikufa kutokana na ugomvi uliotokea kati yake na rafiki yake wa kike Lulu. "Kanumba amefariki usiku wa kuamkia leo (jana) majira ya saa tisa usiku, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni ugomvi kati yake na rafiki yake wa kike anayejulikana kwa jina la Elizabeth Michael 'Lulu' mwenye umri wa miaka 18. Alisema kabla ya ugomvi huo kutokea kati yao wakiwa chumbani, simu ya Lulu iliita na akaamua kutoka nje kupokea kitendo kilichomuudhi Kanumba. Kamanda Kenyela alisema Kanumba aliamua kumfuata Lulu nje huku akifoka kwa sauti akitaka aelezwe kwanini alitoka nje kupokea simu huku akimtuhumu kuwa huenda alikuwa akizungumza na mwanaume mwingine. Aliongeza baada ya Lulu kuona Kanumba akimfuata aliamua kukimbia kutoka nje ya geti , lakini kabla hajafanikiwa kufungua geti, Kanumba alimkamata na kumrudishwa ndani. Kamanda Kenyela, alisema Kanumba akiwa amemshikilia waliingia wote chumbani na kufunga mlango. Hata hivyo, alisema haijulikani nani aliyefunga mlango, ingawa maelezo ya Lulu anadi kuwa aliyefunga mlango ni Kanumba. Kamanda huyo alisema Lulu anaeleza kuwa baada ya Kanumba kufunga mlango, alimuona akilegea na kujigonga kisogo chake kwenye ukuta wa chumba hicho kabla ya kuanguka chini. Alibainisha kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa Kanumba alikuwa amekunywa Whisky (pombe kali) aina ya Jacky Daniel, hata hivyo, bado wanachunguza zaidi kujua kama kweli Kanumba alilegea tu na kuanguka, ama alipigwa na kitu kizito kichwani au alisukumwa kwa nguvu na kumfanya aangukie kisogo. “Uchunguzi ukikamilika tutampeleka mahakamani kwa tuhuma za mauaji,” aliongeza Kamanda Kenyela. Rais Kikwete atoa pole Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania –TAFF kuomboleza kifo cha Kanumba, Katika taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Rais Kikwete ameelezea kushtushwa na kuhuzunishwa na kifo cha msanii huyo ambaye amemtaja kuwa mahiri na mwenye kipaji kikubwa. “Nimepokea kwa mshtuko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Ndugu Steven Charles Kanumba. Kupitia filamu zake, ameburudisha na kuelimisha jamii yetu kwa namna ambayo haiwezi kupimika. Alikuwa msanii mahiri na mwenye kipaji kikubwa ambaye mchango wake mkubwa katika kuanzisha, kukuza na kuimarisha sanaa ya filamu nchini hautasahaulika,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo. Rais Kikwete alisema Kanumba ametoa mchango mkubwa kupitia sanaa ya filamu na kutokana na uwezo mkubwa wa kisanii, Watanzania wataendelea kumkumbuka kwa mchango wake. “Nakutumia wewe Rais wa TAFF salamu zangu za rambirambi na kupitia kwako kwa wasanii wote wa filamu na sanaa nyingine kufuatia msiba huu mkubwa kwa fani yetu ya sanaa. Mama wa Kanumba azungumza Mama mzazi wa Kanumba, Flora Mutegoa amesema alizungumza na Kanumba kwenye simu saa chache kabla ya kifo chake, huku akimtaka arudi Dar es Salaam haraka, kutoka Kagera alikokwenda kumsalimia mama yake (bibi wa Kanumba), ili aje amuage kabla hajasafiri kwenda Marekani. Akizungumza na Mwananchi Jumapili jana katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba wakati akijiandaa kusafi kwenda jijini Dar es Salaam, Flora alisema alizungumza na mwanawe kwa simu usiku huo huo saa chache kabla ya kufikwa na mauti kumkuta. Mama huyo ni mzaliwa wa Kijiji cha Itoju, Kata ya Izigo, Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera lakini kwa sasa anaishi Dar es Salaam . "Mwanangu niliongea naye usiku akiwa mwenye furaha na tulitaniana sana,alisema anatuma nauli nirudi Dar es Salaam tuagane, kwani alikuwa na safari ya kwenda Marekani,"alisema Flora. "Sina cha kuongea naomba mniombee katika kipindi hiki kigumu jana nimeongea naye kwenye simu leo naambiwa mwanangu amekufa,"alisema huku akibubujikwa machozi. Aliongeza kuwa Kanumba aliwahi kumdokeza kuhusu ndoto zake za baadaye kuwa alikuwa na matarajio ya kufika mbali zaidi katika sanaa ya uigizaji. Maneno ya mwisho ya KanumbaSiku za hivi karibuni Kanumba alikuwa akichapisha habari mbalimbali katika mitandao ya kijamii zilizokuwa zikisisitiza upendo. Katika mtandao wake wa Twiter na Blog yake juzi saa sita mchana alichapisha habari akiwasi watu kufanya mambo mema kwa watu wengine ili wapate baraka. "Tunavyofanya kwa ajili yetu huwa yanakufa nasi, lakini tunayoyafaya kwa ajili ya wengine hubaki duniani," sehemu ya maneno yake ya mwisho aliyoyaweka katika Balog yake juzi kabla ya kifo chake . Mbali na ujumbe alioandika siku moja kabla ya kufikwa na mauti, Kanumba amekuwa akichapisha katika mitandoa yake ya kijamii maneno ya busara na kukemea chuki miongoni mwa jamii tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Maneno ya mwisho kwa wasanii wenzakeKanumba mbali ya kutoa maneno ya busara kwa jamii, pia alikuwa akitumia mitandao yake kutoa maneno ya kuwapa moyo wasanii wenzake. Kwa mfano Januari 24 mwaka huu baada ya kutwaa Tuzo ya ZIFF, aliandika kwenye mtandao maneno aliyoyaelekeza kwa wasanii wenzake akisema,: "Maneno yangu ya mwisho, hata tukiwa na uwezo wa kuhamisha milima kama hatupendani katika tasnia ni kazi bure,kile kilicho moyoni ndio kioneshe usoni na si vinginevyo". "Kama wanichukia moyoni basi onyesha usoni na kama wanipenda moyoni basi onyesha usoni na si vinginevyo,Isiwe moyoni wanichukia halafu usoni wanichekea,Hii sanaa ni karama tuliyobarikiwa na Mungu tuitumie vyema kwa ajili ya utukufu wake maana ipo siku atatuuliza na kutudai,kama katupa bure basi anao uwezo wa kutuny'ang'anya pia','soma Wakorintho uone jinsi Mungu alivyogawa karama hizi na ni kwanini katugawia." sehemu ya maneno yake kwa wasanii wenzake nchini. Mamia wafurika nyumbani kwake Mamia ya watu jana walifurika nyumbani kwa msanii huyo kiasi cha barabara ya Sinza Uzuri inayopita karibu na nyumba hiyo kufungwa. Watu kutoka kona mbalimbali za jiji la Dar es Salaam baadhi yao wakiwa wanabubujikwa, machozi walifika kushuhudia kwa macho yao kile wanachokisikia kwenye vyombo vya habari. Kulikuwa na msongamano mkubwa pia wa magari katika eneo hilo. Historia yakeKanumba alizaliwa Januari 8, 1984 mkoani Shinyanga, ni mtoto wa tatu katika familia yao akiwa na dada zake wawili. Alisoma Shule ya Msingi Kaboya, mjini Bukoba na baadaye akahamia Shinyanga ambako alimalizia elimu yake ya msingi katika Shule ya Bugoi. Alijiunga kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari, Christian Seminari iliyopo Kongowe na baadaye akaendelea na masomo ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari ya Jitegemee. Dada wa marehemu Dada wa marehemu, Abela Kajumolo alisema kuwa mipango ya mazishi inafanyika nyumbani kwa marehemu Sinza Vatican. Alisema familia imepanga mazishi ya Kanumba yatafanyika Jumanne wiki ijayo na kwamba bado hawajaamua kama atazikwa Dar es Salaam au Bukoba," alisema. Tayari kamati ya mazishi imeundwa na ikiwajumuisha Gabriel Mtitu, Stephen Jacob (JB) William Mtitu na Issa Mussa (Cloud) ambao wote ni wasanii wa filamu nchini. Kamati ya usafiri itakuwa na Meneja wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba na Vincent Kigosi (Ray). Enzi za Uhai wakeMarehemu alianza uigizaji miaka ya 2000 akiwa na Kundi la Kaole na baadaye kuingia katika fani ya filamu wakati huo akifanya kazi zake chini ya Kampuni ya Game First Quality. Hata hivyo, alifanya kazi na kampuni hiyo hadi alipofanikiwa kumiliki kampuni yake binafsi ya Kanumba The Great Film. Marehemu Kanumba pia ameshirikiana na wasanii wakubwa barani Afrika katika uingizaji akiwamo Ramsey Nouah wa Nigeria ambaye amecheza naye filamu ya Devil’s Kingdom na ambayo imezinduliwa mapema mwezi huu nchini Ghana. Pia hadi mauti yanamkuta, Kanumba alikuwa akiendelea kutengeneza filamu ya Ndoa yangu ambayo alikuwa akiiandaa na mwigizaji mahiri wa kike, Jackline Wolper. Kuingia kwenye siasaMarehemu Kanumba pia katika siku za hivi karibuni aliwahi kukaririwa akisema atagombea Ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, akini hakuweka bayana kupitia chama gani wala jimbo. Kanumba amekuwa msanii wa kwanza nchini kuitangaza Tanzania ndani na nje ya bara la Afrika kupitia filamu. Wasanii wenzake wanasemaje? Suzan Lewis maarufu kama 'Natasha' ambaye ni msanii mkongwe anasema kifo cha Kanumba kimemwachia kumbukumbu ambayo haiwezi kusahaulika. “Nitamkumbuka Kanumba daima katika maisha yangu, alikuwa ni mtu wa watu alikuwa ni msanii pekee aliyepiga hatua na kuishi maisha ya wasanii wa kimataifa. Yvonne Cherryl (Monalisa): “Kifo cha Kanumba kimefifisha ndoto zangu za kuigiza pamoja na wasanii maarufu kutoka Hollywood, tulikuwa na maandalizi hayo na Kanumba ndio alikuwa kila kitu katika suala hilo sikutegemea kama hili lingetokea.” Wema Sepetu: "Siamini, na sitaki kuamini kabisa, nipo ndotoni sijui niseme nini,"alisema Wema huku akiangua kilio kilichomfanya ashindwe kuendelea kuongea. Hatman Mbilinyi: " Alikuwa ni mcheshi sana, alipenda watu waliofanya naye kazi, nimepokea kwa ugumu, siamni kwa sababu ni saa chache tu tulikuwa pamoja, hakuumwa ni bora angeumwa tukajua aliumwa." Jerison Tegete ambaye ni Mchezaji wa Yanga alisema alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kupata habari za msiba, na kwamba ameguswa sana na kifo cha Kanumba. "Inasikitisha sana kwani tumepoteza kijana mdogo na ambaye alikua na nafasi kubwa katika kuielimisha jamii kupitia filamu zake. Single Mtambalike maarufu Richie alisema ana mwachia Mungu kuhusu kifo cha Kanumba. "Sijui nizungumze vipi kuhusu marehemu kwanza siamini kama kweli Kanumba hatutakua naye katika tasnia hii na si filamu tu hata katika kazi nyingine ambazo tumekua naye karibu yote namwachia Mungu.” Jacob Steven amarufu JB alisema ni vigumu kuamini kuwa kanumba kafa kwa vile saa chcahe walikuwa pamoja. “Ni pigo lisiloelezeka kwa sasa na ni vigumu kuamini kilichotokea kwani saa chache kabla ya kifo chake tuliwasiliana na alioongea kwa furaha bila kutambua nini kitatokea mbele yake katika muda mchache ujao.” Tanga na Iringa wamliliaNaye Burhani Yakub kutoka Tanga anaripoti kuwa waandaaji wa filamu wa Mkoa wa Tanga wameleza kuguswa kwao na taarifa za kifo cha Kanumba na kuwataka wasanii wa tasnia hiyo kuwa watulivu katika kipindi hiki cha majonzi. Wakizungumza na Mwananchi Jumapili mara baada ya kusikika taarifa za kifo cha Kanumba jana asubuhi, walisema kifo cha Kanumba ni pigo kubwa kwa tasnia hiyo nchini. Mtunzi Mkongwe wa riwaya na mwandishi wa hadithi za Filam wa Jijini Tanga, Faki A. Faki alisema taarifa za kifo cha Kanumba zimeshtua kwa kuwa ni msanii aliyeikuza sanaa ya filamu nchini. Tumaini Msowoya anaripoti kutoka Iringa kuw Tumaini Msowoya, IringaWakazi wa Mkoa wa Iringa wakiwamo wasanii wa filamu wamesema kuwa wamepokea kwa masikitiko msiba wa msanii nyota wa filamu Tanzania, Steven Kanumba na kwamba taifa limepata pigo kwa kumpoteza mtu muhimu aliyeweza kutangaza filamu za Kitanzania ndani na nje ya nchi. Baadhi ya maduka, kati kati ya mji wa Iringa wameamua kuomboleza kifo cha msanii huyo kwa kutoa nje televisheni zao ili kusaidia watu kuona filamu ambazo zimeigizwa na msanii huyo. Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema msiba huo umewashtua na kwamba msanii huyo alikuwa na mchango mkubwa kwenye sanaa sanaa kupitia filamu zake. Katibu wa kundi la sanaa la Mundu, mkoani Iringa, Athanas Kipera alisema hata kundi lake limepata mchango mkubwa kutoka kwa marehemu Kanumba. Basata wahuzunikaKatibu Mkuu wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) amesema kuwa baraza lake limepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Kanumba."BASATA inaungana na familia za wafiwa na wasanii wote nchini kwa maombolezo ya msiba huu mkubwa na wa kihistoria, kufiwa na msanii huyu mahili kwenye tasnia ya filamu ni pengo kubwa kwa familia, Sekta ya sanaa na Taifa kwa ujumla kutokana na ukweli kuwa, aliweza kuutangaza utamaduni na sanaa yetu nje ya mipaka,"alisema Gonche Materego ambaye ni katibu mkuu wa Basata. Alisema Kanumba atakumbukwa kwa moyo wake wa kujituma na kuthamini kazi ya Sanaa toka akiwa Kundi la Maigizo la Kaole ambapo moyo wake huo ulimfanya awe miongoni mwa wasanii walioleta mageuzi kwenye tasnia ya filamu kwa kuifanya kuanza kupendwa na wadau wengi zaidi. Imeandaliwa na Julieth Kulangwa, Jesca Nangawe, Vicky Kimaro na Phinias Bashaya, Bukoba |
Chanzo: Mwananchi
Un believable lkn ndio ukweli!!!!
ReplyDelete