Wednesday, August 8, 2012

MAJONZI BONGO MOVIES!!!


 
Marehemu Rose enzi za uhai wake.
Odama (katikati) akiaga mwili wa marehemu.
Wolper (wa nne kulia) na jamaa wengine wakiwa msibani hapo.
Hashim Kambi (kushoto) nae akiwa msibani hapo.
Na Erick Evarist
KAMBI ya wasanii wa filamu nchini maarufu kama Bongo Movies imepata pigo zito baada ya kiungo muhimu katika tasnia hiyo, Rose Thomas Maguzo kuaga dunia.
Marehemu Rose aliyefariki Agosti 03, mwaka huu, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikuwa ni mtaalamu wa make up (vipodozi) kwa wasanii mbalimbali nchini.
Taarifa kutoka kwa msemaji wa familia hiyo ilieleza kwamba, marehemu Rose alifariki baada ya kuugua ugonjwa wa homa ya mapafu.
MKANGANYIKO WA MAZIKO
Awali ilielezwa kuwa, marehemu Rose angeagwa Agosti 5, mwaka huu, Muhimbili kabla ya kupelekwa kuzikwa katika eneo ambalo lingetangazwa hapo hapo Muhimbili.
Ndugu, jamaa, marafiki na mastaa wengi wa filamu walifika hospitalini hapo mapema ili kutoa heshima za mwisho kwa mwenzao lakini wakiwa hapo wakaelezwa kwamba mwili utaagwa katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Mabibo – External kwenye misa ya mazishi.

KANISANI HOLA!

Hata hivyo, inaelezwa kuwa baada ya watu kufika kanisani walipoelekezwa hapakuwa na dalili zozote za kuwepo kwa ibada ya mazishi jambo lililowashangaza.
“Unajua tukiwa Muhimbili, mjomba wa Rose (marehemu) alituambia twende kanisani, lakini tukiwa hapo tukasikia tena si hapo, bali msiba unafanyika nyumbani kwa baba wa marehemu Mabibo - Garage, ikabidi tugeuze tena kwenda huko,” alisema mmoja wa wasanii wa filamu ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.
Akaongeza: “Tulipofika nyumbani kwa baba yake tulikuta taratibu za kuaga zinaendelea, lakini kuna baadhi ya wasanii hawakuweza kupata nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho kutokana na kuchelewa.”

MASTAA KIBAO

Baadhi ya mastaa waliohudhuria kwenye mazishi ni pamoja na Jacob ‘JB’ Steven, Single ‘Richie’ Mtambalike, Jacqueline Wolper, Yusuph ‘Angelo’ Mlela na Ruth ‘Mainda’ Suka.
Wengine ni Jenifer ‘Odama’ Kyaka, Rachel ‘Recho’ Haule, Hashim ‘Wingo’ Kambi na wengine wengi ambao walionesha ushirikiano mkubwa katika shughuli hiyo ya kumpumzisha Rose.
Rose alipuzishwa katika nyumba yake ya milele, alasiri ya Jumapili, Agosti 05, mwaka huu, katika Makaburi ya Mabibo.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa, Jina lake lihimidiwe – Amina.
Posted in Globalpublishers

No comments:

Post a Comment