Tuesday, October 2, 2012

Wizi mpya waibuka, watikisa Dar !!!

 
WAKATI wizi wa kutumia silaha ukiendelea kushamiri nchi nzima, sasa umeibuka wizi mpya jijini Dar es Salaam ambapo watu wanaibiwa kwa kushikwa mikono na wezi ambao hujifanya wanafahamiana na wanaowaibia kisha kupoteza fahamu papo hapo.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili wiki hii kwa kuzungumza na baadhi ya ndugu wa watu waliokumbwa na mkasa huo umebaini kuwa, wizi huo hufanywa katika maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa watu kama Mlimani City, majumba ya sinema, klabu maarufu za starehe na kumbi za muziki.

Habari hizo zilieleza kuwa watu hao hufanya wizi huo baada ya kumchanganya mtu akili kwa kushikana naye mkono.

Habari zaidi zinaeleza kuwa watu hao kabla ya kufanikisha wizi huo, humfuatilia mhusika ikiwamo kujua anapoishi, anapofanya kazi na maeneo anayopendelea kwenda pamoja na historia yake na familia yake.

Mbali na habari hizo, hivi karibuni mmoja wa watu walioibiwa kwa mtindo huo, aliandika ujumbe na kuusambaza katika mitandao mbalimbali ya kijamii, ikiwatahadharisha watu kuwa makini na wezi hao.

“Hata ukikutana nao ni vigumu kuwatambua kwa vile wanakuwa wamekufuatilia kwa muda mrefu na kukufahamu kwa kina, hivyo wanapokusimamisha huwezi kuwa na mashaka nao,” anasema mmoja wa watu walioibiwa kwa mtindo huo hivi karibuni.

Kwa mujibu wa ndugu wa watu waliokumbwa na mkasa huo, anayeibiwa hupoteza kumbukumbu mara baada ya kushikana mikono na wezi hao.

Wengi waliokumbwa na utapeli huo walikimbizwa hospitali mara baada ya kuokotwa na wasamaria wema, wakiwa hawajitambui.

Athuman Seleman ambaye ni mkazi wa eneo la Kinondoni, Dar es Salaam aliliambia gazeti hili kuwa aliibiwa mwezi uliopita kwa mtindo huo eneo la Posta Mpya baada ya kuegesha gari lake na alipotoka ndani ya gari alimwona mtu mmoja akiwa amevaa suti akimsogelea huku akimwita kwa kutaja jina lake kuonyesha kuwa anamfahamu.

Selemani alisema alipomfikia alimsalimia kwa kumpa mkono huku akimuuliza habari za siku nyingi kama vile wanafahamiana siku nyingi.

"Nilishangaa kuona mtu huyo akinisogelea huku akiniita kwa kutaja jina langu akitabasamu na kuuliza kwa nini hatuonani siku hizi," alisema Selemani.

Alisema baada ya kusalimiana naye hakumbuki kilichoendelea zaidi ya kujikuta akiwa katika Hospitali ya Muhimbili akipatiwa matibabu.

Selemani alisema baada ya kuzinduka waliompeleka hospitalini walimweleza kuwa baada ya kupoteza fahamu wezi hao walimwingiza ndani ya gari lake na kuchukua vitu mbalimbali zikiwamo pesa, kamera na kadi za benki.

Mkazi mwingine wa jiji ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Peter alisema kuwa anawafahamu watu wawili ambao wameibiwa fedha na vitu mbalimbali kwa njia hiyo.

“Wote ni rafiki zangu ila mmoja aliibiwa mwenyewe na mwingine aliibiwa vitu vyake kupitia kwa mwanaye,” alibainisha Peter.

Alisema kuwa, wiki iliyopita rafiki yake aliibiwa eneo la Mlimani City wakati akitoka kununua vitu mbalimbali na kuchukua fedha benki.

“Alisema waliomwibia walionekana kuwa ni watu wanaomfahamu kwa sababu walimwita jina lake na walipomfikia walimweleza kuwa hawajamwona siku nyingi katika kampuni aliyokuwa akifanya kazi awali,” alisema mtoa habari huyo.
Alifafanua kuwa rafiki yake huyo ambaye alilazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kuokotwa akiwa hajitambui, hakuwa na wasiwasi na watu hao kwa sababu walionekana kuwa wanaomfahamu.

“Walipeana mikono ila wakati akielekea katika gari lake alihisi kupoteza kumbukumbu na watu hao walimkokota mpaka katika gari ambako walichukua Laptop, simu, fedha na kuwatajia namba za siri za akaunti yake bila kujijua,” alisema.
Naye mzazi wa kijana wa miaka 13 aliyeibiwa na wezi hao, ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini aliliambia Mwananchi Jumapili kwamba watu hao walikutana na mwanaye eneo la Buguruni.
“Walivyokutana naye walimsimamisha na kumweleza kuwa ana matatizo, kisha walianza kumwombea kisha walimweleza aende nyumbani kwao akachukue vitu vya thamani ili waviombee,” alisema mama huyo na kuongeza;

“Wakati akiondoka walimpa mfuko uliokuwa na sabuni ndani, alipofika nyumbani alioga na kuchukua simu, hereni, bangili, fedha na vitu vingine vya thamani na kuwapelekea na wakati huo ilikuwa saa tatu usiku.”
Alisema kuwa wakati mtoto wake akichukua vitu hivyo alimwona, lakini alishindwa kumzuia.

Alifafanua mtoto huyo aliporejea alimwambia mama yake jinsi alivyokutana na watu hao mambo yote waliyomweleza na kwamba, baada ya kuifungua mifuko aliyopewa walikuta ndani kuna sabuni na si fedha kama alivyoahidiwa.

Habari zaidi zinaeleza kuwa, matapeli hao pia huwaibia watu wasiowafahamu kwa kujifanya wanaomba kuelekezwa eneo fulani au kujifanya watabiri.

Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa matapeli hao pia wanatumia kadi za biashara ‘Business Card’, ambapo huziweka dawa ambayo humfanya mtu apoteze fahamu mara baada ya kuishika.

“Pia wanatumia mabinti wadogo ambao humweka katika eneo la hatari. Kwa mfano unaweza kumkuta binti mdogo analia sana na kama una gari ukitaka kumpa lifti anakueleza anakoishi. Ukimpeleka utawakuta wenzake ambao wanaweza kukupora gari na vitu vingine ulivyonavyo,” alisema mkazi mmoja wa Mwananyamala, Jimmy Seka.

Kauli ya Polisi
Kamanda wa Polisi wilaya ya Kinondoni, Charles Kenyela alisema hajapata taarifa za matukio hayo na kuongeza kuwa wizi wa aina hiyo unaweza kutokea na kuwataka wananchi kuwa waangalifu.

Kenyela alisema eneo la Mlimani City limekithiri kwa uhalifu licha ya kuwapo kampuni binafsi za ulinzi zinazolinda eneo hilo.

Alifafanua kwamba, wamiliki wa hoteli na maduka makubwa wanatakiwa kuweka kamera zitakazoangalia mienendo ya watu, ili kuwabaini wezi uhalifu unapotokea.

Naye Kamanda wa Polisi Wilaya ya Temeke, David Misime alisema katika kanda yake hajapokea kesi za aina hiyo na hajawahi kuisikia.

“Kwa upande wa Temeke sijawahi kusikia wizi wa aina hiyo, labda kama wanaoibiwa hawatoi taarifa katika vituo vya polisi,” alisema Misime.

Naye Kamishna Msaidizi wa Polisi Wilaya ya Ilala, Marietha Milangi alisema pamoja na kuwa hajasikia tukio hilo, atafanya juhudi za kufuatilia ili kubaini ukweli.

“Nitafuatilia kwa ukaribu ili kujua kama ni kweli na endapo nikipata taariza hizo nitaziweka wazi kwa wananchi,” alisema Malangi.

Ofisa Habari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Eminael Aligaesha alisema hana taarifa zozote endapo kuna mgonjwa wa aina hiyo aliyefikishwa hapo.

“Leo ni Jumamosi na sina taarifa za aina hiyo labda nitafute Jumatatu (kesho) nitakuwa nimeshauliza kwa wanaohudumia wagonjwa ili kujua kama kuna mgonjwa wa aina hiyo aliyefikishwa hapa,” alisema Aligaesha.
Chanzo:Mwanachi

No comments:

Post a Comment