Friday, July 20, 2012

YALIYOJIRI MAGAZETINI


MAMA KANUMBA AMVAA MAMA LULUMama Kanumba, Flora Mtegoa.
Mama Lulu, Lucresia Karugila.
Marehemu Steven Kanumba.
Elizabeth Michael ‘Lulu’.
Hamida Hassan na Gladness Mallya
CHOKOCHOKO zimeanza! Huku kesi ya kifo cha mwanaye ikiendelea na Elizabeth Michael Kimemeta ‘Lulu’ akisota nyuma ya nondo za mahabusu ya Segerea, mama mzazi wa marehemu Steven Charles Kanumba ‘The Great’, Flora Mtegoa amemvaa mama Lulu, Lucresia Karugila, Ijumaa linafunguka.
MANENO MAZITO YA AIBU
Kwenye mahojiano maalum na gazeti hili nyumbani kwake Kimara-Temboni, Dar es Salaam, mapema Jumanne wiki hii, mama Kanumba alimtolea mama Lulu maneno mazito huku akimshangaa kwa kushindwa kumpa pole na kumfariji tangu mwanaye afikwe na umauti Aprili 7, mwaka huu.
Mama Kanumba alisema anaongea kwa uchungu kwani hakutegemea kama mama Lulu anaweza kuwa kimya mpaka leo hii bila hata kumpa pole wakati matatizo yamewakuta watoto wao wote.


TUPATE SAUTI YA MAMA KANUMBA 
Ijumaa: Ili kupata kile alichokisema mzazi huyo mbele ya gazeti hili, tujiunge naye akiwa nyumbani kwake Kimara-Temboni. 
Kwako mama Kanumba: Namshangaa sana mama Lulu kwani namuona kama siyo mzazi mwenzangu. Huwezi amini mpaka leo hii hajawahi hata kunipa pole wala kunitumia ujumbe wa watu kunifariji, hivi anategemea mimi nimfuate? Yeye mwanaye yupo hai wangu ndiyo ametangulia. Nimeona niseme kabisa nimpe habari yake.
Ijumaa: Kwani wewe uliwahi kufanya jitihada za kukutana na kufarijiana naye akakataa?
Mama Kanumba: Mama Lulu siyo kabisa. Aliwahi kufuatwa na kuombwa ushirikiano wakati kesi imefunguliwa akakataa. 
Ijumaa: Mbona kuna madai kuwa baada ya kifo cha Kanumba upande wa Lulu ulikufuata ukakataa kutoa ushirikiano?
Mama Kanumba: Sijawahi kuongea na mtu yeyote wa upande wa Lulu. Huyo anayedai alikuja kuniomba ushirikiano nikamfukuza ananisingizia kwani simfahamu Lulu na mama yake zaidi ya kuwaona kwenye vyombo vya habari na filamu (Lulu).
Ijumaa: Je, akikufuata utamkubalia aje kukufariji?
Mama Kanumba: Mimi sina nia mbaya na mama Lulu, kibinadamu namuona kakosea kwani kama yeye alikuwa akiogopa, angetuma watu waje kwa niaba yake. Nilidhani alikuwa akiogopa kuja Sinza (Vatican kwa Kanumba) kwa sababu ya waandishi lakini hata nilipohamia huku (Temboni) hajaja. Ukweli ni kwamba akija nitampokea tu ila sidhani kama ipo siku atakuja, nawashangaa hata washauri wake.
Ijumaa: Unaizungumziaje filamu ya Foolish Age ya Lulu ambayo Kanumba aliipeleka Steps?
Mama Kanumba: Ni kweli filamu hiyo ipo Steps, Kanumba ndiye aliipeleka kwa nia ya kumuinua Lulu lakini kabla haijalipwa mauti yakamkuta. Ingekuwa ya Kanumba ningefuatilia. 
Baada ya mahojiano hayo, Ijumaa lilitafuta mzani upande wa pili wa mama Lulu ambapo mahojiano yalikuwa hivi:


TUJIUNGE NA MAMA LULU AKIWA TABATA
Ijumaa: Mama Lulu gazeti la Ijumaa limezungumza na mama Kanumba anakulaumu kwa kushindwa kumfariji baada ya kifo cha mwanaye Kanumba aliyekutwa na umauti akiwa na Lulu. Je, unalizungumziaje suala hili?
Mama Lulu: Eehee unasemaje? Wewe ni nani? Mwandishi? Nimeshawaambia mniache kabisa kwani bila habari ya Lulu na Kanumba hamuuzi?
Ijumaa: Katika maadili ya kazi yetu mtu mmoja akiongea lolote juu ya mwenzake lazima pande zote zisikilizwe hivyo hii ndiyo nafasi yako. Unalizungumziaje suala hilo la mama Kanumba? 
Mama Lulu: Sitaki kushauriwa na wewe mwandishi, nina washauri wazuri tu tena ni watu wazima, tafadhali naomba mniache nipumzike.


KIFUATACHO
Bado kesi ya Lulu ni mbichi ambapo itaendelea kuunguruma baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kumaliza utata wa umri na jina la Lulu Julai 23, mwaka huu.


KALAMU YA IJUMAA
Wazazi hawa wanapaswa kuwa na staha kwa sababu kila upande una machungu. Kanumba hatunaye na Lulu yupo nyuma ya nondo. Ni vyema wakakaa chini bila kukorogana ili kupunguza machungu waliyonayo.

WEMA, DIAMOND WANASWA KIGOMA


Nasib Abdul Juma ‘Diamond’.
Wema Isaac Sepetu.
Na Shakoor Jongo
STAA wa filamu Bongo, Wema Isaac Sepetu na kichwa kinachotingisha katika Bongo Fleva, Nasib Abdul Juma ‘Diamond’ wamenaswa wakiwa beneti mkoani Kigoma, Ijumaa lina data kamili.
Chanzo makini kilichopo mkoani humo, kimepenyeza habari hiyo kwa paparazi wetu kwa njia ya simu juzi, ambapo kilisema ukaribu wao uliamsha hisia kwamba huenda wawili hao wamerudiana.
“Wapo wote huku Kigoma, kwa Diamond ni sawa maana yupo na wasanii wenzake wa Kigoma All Stars, sasa Wema amekujaje? Kwanza siyo mwanamuziki, lakini pia siyo mtu wa Kigoma ni wa kutoka Tabora,” kilieleza chanzo hicho.
Baada ya kupata habari hiyo, Ijumaa lilimvutia waya Diamond zaidi ya mara tatu lakini simu iliita bila kupokelewa.
Wema alipopigiwa simu alipatikana na kufafanua ishu nzima ilivyo. Huyu hapa msikie: “Ni kweli nipo huku Kigoma lakini sipo na Diamond. Nimekuja kwa mwaliko wa Zitto Kabwe (Mbunge wa Kigoma Kaskazini).
“Mimi na Diamond ni marafiki tu, hatuwezi kuwa wapenzi tena, kila mtu na maisha yake. Kifupi nina mtu wangu ambaye tunapendana na kuheshimiana sana.”
Alipotakiwa kumtaja mpenzi wake mpya alisema: “Kwa sasa siwezi kumtaja, lakini siku si nyingi nitamuweka hadharani watu wamjue.”

DOTNATA ABADILI DINI


Husna Posh ‘Dotnata’.
Hamida Hassan na Gladness Mallya
MSANII mkongwe katika tasnia ya filamu za Kibongo, Husna Posh ‘Dotnata’ amebadili dini kutoka Uislam na kuwa Mkristo kwa kile alichodai ni kutengeneza maisha yake baada ya kuhangaika na mambo ya dunia kwa muda mrefu.
Akichezesha taya na Ijumaa, Dotnata alisema amefikia uamuzi huo baada ya kuugua na kuhangaika kwa waganga wengi kwa muda mrefu bila ya mafanikio.
Dotnata ametaja sababu nyingine ni mama yake mzazi ambaye alifikia hatua ya kususa kumtembelea nyumbani kwake hasa kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani akimtaka aokoke.
“Mama alinipa masharti kwamba nitakapookoka ndipo atakapofika kwangu jambo ambalo lilikuwa linaninyima amani na kunifanya nichukue uamuzi huo,” alisema.
Dotnata ambaye awali alikuwa ni Mkristo amebatizwa upya na anatumia jina lake la awali kabla ya kuwa Muislam la Iluminata na amejiunga na Kanisa la Ufufuo na Uzima (kwa Gwajima) lililopo Kawe jijini Dar.
“Nitakuwa nahudhuria kanisani siku tatu kwa wiki kwa ajili ya kujifunza neno, pia nyumbani kwangu nimetenga sehemu maalum kwa ajili ya kuangalia mahubiri ya mtumishi wa Nigeria TB Joshua kwa njia ya runinga,” alisema.
Dotnata amesema kuwa ameapa kutogeuka tena kwani ataendelea na wokovu wake mpaka dakika ya mwisho wa maisha yake ili atakapozikwa ndugu na jamaa zake wacheze sebene la Yesu.
“Naomba niliowakosea wanisamehe kwani wengine nimeshawapigia simu na kuwaomba radhi, hivyo natumia fursa hii kuwaomba wengine wote wanisamehe kwa sababu nimeanza maisha mapya,” alisema Dotnata.
Alipoulizwa kuwa mumewe Posh amelipokea vipi suala la kuokoka kwake, Dotnata alisema mumewe hana matatizo na anaona ni jambo la kawaida na maisha ya upendo na amani yanaendelea kutawala ndani ya ndoa yao.

Posted in global publishers

No comments:

Post a Comment