Mwanafunzi
wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Mbondole, Kata ya
Msongola, Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, Neneu Baltazar,
anatuhumiwa kuchoma kisu mwalimu wake, Frank Gama, baada ya kuzuka
vurugu shuleni hapo.
Vurugu
hizo zilitokea baada ya mwanafunzi wa kike kuibiwa simu yake ya
kiganjani na kumhisi mwanafunzi mwenzake Neneu kuwa ndiye aliyehusika na
wizi huo.
Hata hivyo, Neneu alipokataa, ndipo vurugu zilipoibuka kati ya wanafunzi hao wawili.
Akisimulia
mkasa huo, Mwalimu Gama alisema baada ya kuona wanafunzi hao
wanagombana, alichukua jukumu la kwenda kuamulia ugomvi huo.
Hata hivyo, alisema wakati akifanya hivyo, ghafla alijikuta akichomwa kisu mgongoni.
“Vijana
hao wamenipiga sana lakini isingekuwa walimu wenzangu kuja kuniokoa,
sijui ingekuwaje. Kwani walikuja kama nyuki nimeumizwa na sasa nakwenda
Hospitali ya Taifa Muhimbili kutibiwa,” alisema Mwalimu Gama.
Makamu
wa Mkuu wa shule hiyo, Juma Robinson, aliliambia NIPASHE jana kuwa
vurungu hizo zilisababishwa na utovu wa nidhamu wa wanafunzi wa shule
hiyo.
Alisema
vurugu kama hizo za kupigwa walimu shuleni hapo, ni jambo la kawaida
kwani hata yeye aliwahi kupigwa ngumi lakini hakuna hatua zozote
zilizochukuliwa.
Hata
hivyo, Juma alisema tukio hilo la jana walitoa taarifa polisi jamii wa
mtaa huo ambao walifika na kumkamata mmoja wa wanafunzi hao lakini
wengine walikimbia.
“Utovu
wa nidhamu katika shule za kata zinasababishwa na kutokuwa na bodi za
shule na maamuzi katika kila shule huachiwa mtu mmoja," alisema.
Kamanda
wa Polisi Jamii katika mtaa huo, Richard Mosoba, alisema walipofika
eneo hilo, walimkamata mwanafunzi huyo na kumfikisha katika kituo cha
Polisi cha Stakishari Ukonga.
“Sisi
tulijitahidi kutimiza jukumu letu la kumfikisha mtuhumiwa aliyemchoma
kisu mwalimu, lakini nini kitafuatia, hiyo ni kazi ya polisi. Kwanza
hatuna silaha zaidi ya pingu, sasa unategemea nini kitokee kwenye
vurugu?,” Alihoji Mosoba.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Ilala, Marietha Minandi, alithibisha kutokea kwa tukio hilo.
Alifafanua
kuwa ugomvi huo uliwahusu wanafunzi na kidato cha tatu na cha nne baada
ya mwanafunzi mmoja kuibiwa simu na kumhisi wa kidato cha nne kuwa
ndiye aliyeiba.
Alisema
wanafunzi walipigana na baadhi yao wakamua kumuita mwalimu aende
kuwaamulia lakini alipofika mwanafunzi mmoja alichoma kisu.
Mwanafunzi huyo kwa sasa anamshikiliwa polisi kwa kwa mahojiano.
CHANZO: KULIKONI
No comments:
Post a Comment