Tuesday, November 6, 2012

WACHUNA NGOZI WAIBUKA UPYA IRINGA
TUKIO la kusikitisha limetokea hivi karibuni katika Kijiji cha Wenda, Kitongoji cha Lupeta, mkoani Iringa kwani umekutwa mwili wa mwanakijiji aliyetambulika kwa jina la Leonard Kutika (49) ukiwa umechunwa ngozi, hivyo kuvuta hisia kuwa wachuna ngozi wameibuka upya.
Mwili wa marehemu Leonard Kutika (49) ukiwa umechunwa ngozi.
Licha ya kuchunwa ngozi, marehemu alikuwa amenyofolewa macho pamoja na kukatwa sehemu zake za siri.
Akizungumza na gazeti hili, baba mdogo wa marehemu Leonard, Martin Kutika mkazi wa Lupeta alikuwa na haya ya kusema: “ Siku ya tukio nilipigiwa simu usiku na ndugu yetu aitwaye Kibadeni aliyesema kuwa Leonard alikuwa akisumbuliwa na tatizo la akili alikutwa katika nyumba aliyokuwa anaishi huku akiwa amefariki na kuondolewa sehemu za siri na kuchunwa ngozi.
“Ndugu yangu Zawadi Mwenga alikuwa mmoja wa watu wa kwanza kwenda eneo la tukio na kukuta kweli Leonard amefariki.”
Mwenga naye alikuwa na haya ya kusema: “Siku mbili kabla ya tukio marehemu alionekana mitaani lakini baada ya hapo hawakumuona tena hadi alipogunduliwa na mwanamke mmoja akiwa amefariki dunia.”
 Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Wenda,  Dismas Ngweta alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na kusema kuwa alitaarifiwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Lupeta, Geofrey Dugange.

Wanakijiji wa Wenda, Kitongoji cha Lupeta, mkoani Iringa wakiwa na hofu kuhusiana na tukio hilo.
Alisema alikwenda eneo la tukio na walipouangalia mwili wa marehemu waligundua kuwa ulichunwa ngozi, kunyofolewa macho, kukatwa sehemu za siri pamoja na kutobolewa katika sehemu ya mguu.
Ngweta ameeleza kuwa baada ya kupata taarifa ya tukio hilo, aliwaarifu Polisi wa Kituo cha Ifunda ambao hata hivyo, mpaka mwandishi wa habari hizi anaondoka eneo la tukio walikuwa hawajafika.
Tukio hilo la mauaji ni la pili kutokea kijijini hapo baada ya Septemba 25, mwaka huu kuuawa kinyama dereva wa bodaboda na pikipiki yake kutoonekana
chanzo; GPL

No comments:

Post a Comment