Sunday, April 29, 2012

TAMKO RASMI KUHUSU SHUTUMA DHIDI YANGU JUU YA KIFO CHA KANUMBA

Yapata wiki tatu sasa tangu msanii mwenzangu Steven Kanumba aage dunia, na kama ilivyo kwa kila kitu kinapotokea huandamana na kila aina ya maneno na hisia mbali mbali kutokana na mitazamo ya watu kupishana kuhusiana na jambo husika. Kulingana na muktadha huo, msiba wa Steven Kanumba umekumbwa na maneno na hisia kama hizo, hususan mazingira ya kifo chake; kinachosikitisha zaidi watu wengi (ambao wanajitambulisha kama wapenzi wa Kanumba), na baadhi ya vyombo binafsi vya habari vimekuwa vikinihusisha na kifo hicho, kwa kusema kwamba kwa njia moja au nyingine ninahusika na mauaji ya Steven Kanumba. Kwa muda wote huo tangu msiba ulipotokea mpaka leo hii nashika kalamu kujaribu kuyaweka sawa na kuondosha hisia chafu katika fikra za watu, nimekuwa nikipitia katika wakati mgumu sana kwa jinsi ambavyo nimekuwa nikinyooshewa vidole kila upande nikihusishwa na kifo hicho, kiujumla nimezingatia maoni ya wapenzi ya mashabiki wangu wakinitaka kuwa na subira, ila kuna ukweli usemao kwamba, uongo ukirudiwa sana jamii huusadiki na kuuona ukweli, nimeona nisikae kimya ila niweke sawa hili kwamba sihusiki na kifo cha Steven Kanumba.
Nasema wazi kwanza sihusiki kabisa na kifo cha Kanumba kwanza kwa kuzingatia mazingira yenyewe ya kifo kilivyotokea. Wakati kifo hicho kinatokea, nilikuwa sehemu nyingine kabisa na mimi nilikuwa mtu wa tatu kutaarifiwa kwamba Kanumba amepatwa na mkasa ambao baadae ulisababisha kifo chake. Na na hata nilipofika katika hospitali ya Muhimbili (tofauti na watu wanavyodhani kuwa nilifika nyumbani kwake; ukweli mimi nilimkuta tayari amepelekwa Muhimbili), nilikuta tayari alikuwa ameshafariki ndio maana hata Polisi wanaohusika na usalama wa raia, si tu kwamba hawakuniweka chini ya ulinzi, sikuitwa hata kuhojiwa kwa sababu hakuna mazingira yoyote yanayonihusisha mimi na kifo hicho.
Pili, watu wanahusisha tofauti za kibinadamu zilizokuwepo baina yetu na kifo hicho, nasema hii sio sahihi kwa sababu kwanza ni kawaida kwa binadamu kutofautiana, isipokuwa kwetu sisi baadhi ya vyombo vya habari vilikuwa vinakuza kwa sababu nisizozijua, hivyo jamii ikachukulia kuwa tofauti zile ni uadui kitu ambacho sio sahihi, kwani sisi hatukuwa watu pekee tunaotofautiana kwani huu ni mwenendo wa kawaida wa dunia; hivi jana tumeshuhudia Waziri mmoja akieleza bayana katika mkutano na waandishi wa habari kuwa na tofauti na naibu wake, lakini hatuajasikia ikiandikwa wana ‘bifu’ bali imetafutwa lugha nzuri ya kupamba tofauti hizo, kwa kuwa waliohusika ni waheshimiwa, ila kwa wengine kutokana na sababu tusizozijua, inaonekana kama ni haki yetu kuandikwa vibaya. Kinachosikitisha, kwa nini jambo hili linachukuliwa kwa mkazo mkubwa sana, kwani hatujawahi kusikia watu wakiwa wanatofautiana na ndugu jamaa hata na marafiki zao na inaonekana kawaida tu? Kwani vyombo vya habari havikuwahi kuandika kuwa marehemu Steven Kanumba alikuwa na tofauti na baba yake, na yeye mwenyewe alitamka hivyo katika vyombo vya habari, mbona wameliongea bila kuongeza chumvi, na jamii inaona kuwa ni jambo la kawaida la kibinadamu.
Pengine watu wanaojaribu kuongea hayo, hawajui mimi na Steven Kanumba tumetoka wapi? Sisi si watu tuliokutana barabarani, tuna historia katika kazi yetu ya sanaa na pia katika maisha maisha yetu. Mwanzoni kabisa, mimi ndiye niliyempokea Kanumba pale Kaole na ndiye niliyemfundisha sanaa pale (nadhani watu wanakumbuka tamthiliya za wakati huo ITV) na baada ya hapo tulienda pamoja katika kampuni ya Game 1st Quality pamoja na tukafanya filamu kama Johari, Sikitiko Langu, Dangerous Disire na nyinginezo, na tuliendelea kuwa pamoja katika kampuni hiyo mpaka tulipofanya filamu ya Oprah mwaka 2008 ambapo niliingia rasmi kufanya kazi za kampuni yangu, lakini tuliendelea kuwa pamoja hata wakati nikiendelea na kazi za kampuni yangu. Pia mimi nilikuwa wa kwanza kuanza kufanya kazi na Steps na baadae Kanumba alipoanza kufanya kazi zake mwenyewe na kunikuta huko tuliendelea kuwa pamoja kama siku zote. Kitu kikubwa kilichokuwa kinaendelea baina yetu, ni kwamba tulijenga ushindani wa kuendeleza kazi mbele kwa kila mmoja akitoa kazi, mwingine anamjibu, Isitoshe hata vitu vyetu binafsi utaona kama kuna kufanana; kuna wakati Kanumba alinunua Toyota Ruv 4 nyeusi mimi nikanunua ya kijani, aliponunua Harrier na mimi nikanunua pia, na hata gari za hivi karibuni, ukitazama utaona kuwa zinafana kwa karibu; hii ilikuwa ni kama maisha yetu, hatukuwa na uadui, ilikuwa tunapeana changamoto za maendeleo.
Watu wanaojaribu kuonesha kuwa tofauti zetu ilikuwa ni uadui, huwa hawajui wapi tulikotoka ndio maana wanasema wasemavyo na katika kuthibitisha kuwa tofauti hizo hazikufikia katika uadui, kuna watu ambao wanafanya kazi nami katika kampuni yangu ya RJ ndio hao hao Kanumba alikuwa anawatumia siku zote katika kazi zake, hata baada ya tofauti hizo hakuna aliyekoma kufanya kazi na yeyote kati yetu. Hii inathibitisha kuwa tofauti ilikuwa kati yetu kama binadamu, sio chuki za kimafanikio, ingekuwa hivyo watu kama Junior Syaary ambaye mara nyingi hufanya final editing katika RJ ndio huyo huyo alikuwa akifanya na Kanumba, Ally Yakuti ambaye anaandika script za RJ, ndiye huyo huyo aliyekuwa anaandika kwa Kanumba, Steven Shoo ambaye ni mtaalamu wangu wa light, ndiye huyo huyo anayetumiwa na Kanumba na wengine wengi kama Juma Chikoka aliyecheza kikamilifu katika filamu ya kijiji cha Tambua Haki, ambaye pia anashiriki filamu nyingi za RJ, na wote hao, hawakuanzia kwa Kanumba, wote wameanza kwangu mimi ndio niliompatia na hata baada ya hayo yanayosemwa kuwa kuwa ni uadui, sikuwahi kuwakataza kufanya kazi na Kanumba.
Tatu kumtuhumu mtu kwa namna yoyote ile bila ya uthibitisho wa tuhuma hizo, ni kosa kwa sheria za nchi na pia kama ni mfuasi wa dini yoyote ni dhambi, kwani wakati ukisema hayo huku hujui uhalisia bali unasukumwa na nguvu za hisia tu ni sawa na kumchafua mtu huyo katika jamii bila ya kujua jamii inamchukuliaje. Napenda kusema wazi wazi kuwa, kwa kila anayetekwa na wimbi hili, ajaribu kufikiria leo ipo kwangu mimi, kesho inaweza kuhamia kwako, kwani mimi sio wa kwanza kufikwa na haya, inaweza kukukuta hata wewe au ndugu yako, utajisikiaje. Na kama kweli mimi nimehusika na kifo cha Kanumba kwa namna yoyote ile, basi Mungu atanihukumu na kila aliye hai atashuhudia, ila kama sijahusika kwa lolote, Mungu hatonihukumu na badala yake ataniinua, kwa kuwa ninapita katika kipindi kigumu mno sasa hivi kwa madhila haya.
Mwisho kabisa napenda kumaliza kwa msemo usemao, ajidhaniaye amesimama, aangalie asianguke, kwani kadri mambo haya yanavyoendelea, usidhani yataishia kwangu, kwani mkono wa dhuluma haushii karibu, ukisikia jirani anapiga kelele za mwizi, usilale kamsaidie, usiseme kuwa hatuhusiki kwani hayupo kwetu, kesho utafikwa na wewe utakosa wa kukusaidia. cha msingi kama tunampenda sana ndugu yetu ni kumuombea kwa Mungu, kwani hatujui makao yake huko aliko, na sio kuunda vitu ambavyo kamwe hata yeye angekuwa hai asingeviafiki.
MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU STEVEN KANUMBA MAHALI
PEMAPEPONI
MUNGU IBARIKI AFRIKA MUNGU IBARIKI TANZANIA

No comments:

Post a Comment