Sunday, May 20, 2012

MABANGO YABANDIKWA KUMSAFISHA NGELEJA!


Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini,William Ngeleja  

Na Frederick Katulanda, Geita
MABANGO yenye lengo la kumsafisha aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja yamebandikwa katika sehemu kadhaa katika Jimbo lake la Sengerema, Mwanza.Habari zilizopatikana jana mchana kutoka Sengerema zinasema mabango hayo yalianza kubandikwa juzi usiku na watu ambao walikuwa wakitumia gari.
Ngeleja ni mmoja wa mawaziri sita walioachwa katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri wiki mbili zilizopita na katika uongozi wake amekuwa akituhumiwa kwa kushindwa kumaliza tatizo la umeme, ufisadi wa fedha za umma katika sekta za nishati na madini.
Mabango yanayomsafisha mbunge huyo ni kivuli (photocopy) cha moja ya kurasa za gazeti linalotoka mara moja kwa wiki, ambalo lilichapisha makala yenye kichwa cha habari kisemacho: ‘Zito Kabwe amsafisha Ngeleja.”
Maudhui ya makala hayo yanamsafisha Ngeleja kwamba hahusiki na kashfa ya ufisadi wa Sh600 bilioni ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambayoo ni moja ya sababu zilizomfanya mbunge huyo kutupwa nje ya Baraza la Mawaziri.
Mmoja wa wakazi wa Busisi wilayani Sengerema, Barnabas Mango alisema: “Haya makaratasi yamebandikwa na wafuasi wake (Ngeleja), wamefika hapa jana (juzi) jioni na kuonana na baadhi ya vijana, wakawapa Sh30,000 wakaachia nakala nyingi na kuambiwa wabandike kila kona ya kijiji hiki, nadhani ameamua kutafuta huruma kwa wananchi ili aonekane kwamba hana hatia.”
Hata hivyo, Ngeleja alisema jana kuwa hafahamu chochote kinachoendelea jimboni kwake wala hajamtuma mtu yeyote kubandika matangazo ya kumsafisha kwa kuwa yuko Dar es Salaam.
“Sijui chochote kuhusu suala hilo wala sijamtuma mtu kwenda kunisafisha jimboni kwangu,” alisema Ngeleja kupitia ujumbe mfupi wa simu yake ya mkononi na kuongeza:
“Mimi sijui kinachoendelea huko jimboni kwani bado niko Dar es Salaam na hivyo siwezi kujua kinachoendelea huko. Hakuna mtu niliyemtuma akabandike vipeperushi hivyo.”
Maudhui yake
Mabango hayo yanawanukuu baadhi ya watu akiwamo Zitto kwamba walisema kuwa ufisadi wa Sh600 bilioni ndani ya Tanesco ambao Ngeleja anadaiwa kuufumbia macho si wa kweli na kwamba hakuna senti hata moja ambayo imefujwa ndani ya shirika hilo katika mwaka unaotajwa na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2009/2010.
Bango hilo inaeleza kuwa tuhuma zote za ulaji wa fedha ndani ya Tanesco zilikuwa za ‘kupikwa’ kwa lengo la kumng’oa Ngeleja na kwamba si wizara yake wala Tanesco waliokuwa wametajwa kwenye Ripoti ya CAG na ile ya Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC), inayoongozwa na Zitto kwamba wanahusika na matumizi mabaya ya fedha za umma zilizodaiwa kuwa kati ya Sh300 bilioni na Sh600 bilioni.
“Badala yake, katika mwaka huo a fedha 2009/2010 ambao ripoti ya CAG iliyojadiliwa na bungeni na kuzua mtafaruku mkubwa uliowashinikiza baadhi ya mawaziri kujiuzulu, shirika hilo la ugavi lilipata hati safi toka kwa CAG…..,” inasomeka sehemu ya taarifa kwenye bango hilo na kuongeza:
“Kutajwa kwa Ngeleja katika kashfa ya Tanesco ulikuwa ni mpango maalum unaodaiwa kuratibiwa na mbunge kijana ndani ya CCM, ambaye alishirikiana na baadhi ya mawaziri kupenyeza taarifa za uongo kwa mmoja wa waandishi wa habari wa chombo kimoja nchini kwamba anapaswa kuwajibika…”
Aidha, bango hilo linaeleza kuwa katika kuhakikisha kuwa tuhuma za Ngeleja zilikuwa za kupikwa, Zitto na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, William Mhando wamekaririwa kwa nyakati tofauti na baadhi ya vyombo vya habari wakieleza upotoshaji kuhusu taarifa hizo ambazo zilisababisha Ngeleja kuhukumiwa kwa kuachwa kwenye mabadiliko ya Baraza la Mawaziri.
Mabango hayo pia yameonekana kubandikwa katika nguzo za umeme katika maeneo ya Nyampulukano, Tunyenye na Kituo cha Mabasi cha Sengerema Mjini.
Mkazi wa Nyampulukano, Said Juma alisema ameshuhudia wananchi kwa makundi walisoma mabango hayo Mjini Sengerema.
“Kujisafisha huku hakutamsaidia kwa ni Watanzania wa leo wameamka na tunajua kuwa Ngeleja aliachwa katika Baraza jipya la Mawaziri kutokana na nini. Mbona naibu wake ameachwa? Hii ni lazima alihusika kwa namna moja au nyingine,” alisema.
Mkazi wa Mamanzini, Edward Maganda alisema alishuhudia baadhi ya wananchi wakichana mabango hayo baada ya kubandikwa katika sehemu mbalimbali za eneo hilo.
“Mimi naona ana haki ya kujieleza iwapo amechafuliwa kwa hila, lakini maeneo mengine kama huku kwetu wanayachana, hawamtendei haki kwa kuwa wanawanyima wapiga kura wake haki ya kufahamu ukweli,” alisema Maganda.
Mkazi mwingine, Mwanne Ibrahimu alisema katika eneo la Kamanga Feri wananchi walikuwa wakipigania kupata nakala za mabango hayo yaliyokuwa yakigawiwa na vijana ambao hawafahamu.
“Wakati natoka Mwanza kwenda Sengerema niliwaona vijana pale Kamanga Feri wanagawa hayo makaratasi na mimi nilipata nakala yangu na watu walikuwa wanagombania, ila sijui kama ataweza kusambaza jimbo zima,” alisema.

chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment