Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hamad Masoud Hamad (pichani) amejiuzulu wadhifa wake jana kufutia ajali ya kuzama kwa meli ya Skagit.Taarifa ya Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Abdulhamid Yahya Mzee ilisema tayari Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein amekubali ombi la kujiuzulu kwa Waziri Hamad.
“Tarehe 20 Julai, 2012 Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Mheshimiwa Hamad Masoud Hamad alimuandikia barua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimia Dk Ali Mohammed Shein kumuomba ajiuzulu kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya Mv Skagit iliyotokea Julai 18,2012,” Ilisema taarifa ya Dk Mzee.
“Kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Rais amemteua Rashid Seif Suleiman kuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano,” Taarifa ya Ikulu ilisema na kwamba Uteuzi wa Waziri mpya huyo umeanza Julai 23 mwaka huu.
Wakati huo huo, Dk. Ali Mohammed Shein ameunda Tume ya kuchunguza ajali ya kuzama kwa meli ya Mv Skagit ambayo itaongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Abdulhakim Ameir Iss.
Wajumbe wa tume hiyo ni Meja Jenerali S.S. Omar, Hassan Mussa Mzee, Kapteni Abdulla Yussuf Jumbe, Kaptein Abdulla Juma Abdulla, Salum Taoufiq, Kaptein Hatibu Katandula, Mkali Fauster Ngowo, Ali Omar Chengo na Shaaban Ramadhan Abdalla ambaye ni Katibu wa Tume.
Mapema akizungumza na waandishi wa habari mjini Unguja jana, Makamu wa Pili wa Rais wa SMZ, Balozi Seif Ali Iddi alisema lengo la kuundwa kwa tume hiyo ni kupata ushauri wa nini cha kufanya katika kuhakikisha vyombo vya abiria vinakuwa salama.
Balozi Iddi alisema kutokana na hali ya ajali zinazotokea na mbali na Tume hiyo, Serikali imeona kuwa ipo haja pia ya kupitia upya Sheria zinazohusu usafiri wa baharini na kuweka aina ya viwango vya meli zitakazoruhusiwa kuingizwa nchini na kuchukua abiria.
Alisema pia Serikali unakusudia kununua meli kwa ajili ya usafiri ipo palepale na kwamba, juhudi zinaendelea katika kufanikisha suala hilo.
"Katika hatua ya kudhibiti majanga ya aina hii, Serikali inakusudia kuzifanyia mapitio sheria zinazohusu usafiri wa bahari na kuweka viwango vya aina ya meli zitakazoruhusiwa kuingizwa nchini na kuchukua abiria,” alisema.
Kauli ya CUF
Mapema jana Mwenyekiti wa CUF, Profea Ibrahim Lipumba alisema alitumaini kuwa Hamad angechukuwa hatua kwa kuzingatia mfululizo wa ajali hizo.
Profesa Lipumba alisema waziri huyo anayetokana na Chama cha CUF, anapaswa kuwajibika ili kumsaiddia Rais na Serikali kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
“Chama kina imani kuwa atawajibika kwa kilichotokea,” alisema Lipumba.
Alisema kimsingi waziri huyo hana kosa la kiutendaji, lakini hali halisi ya kisiasa, inamtaka kuchukua hatua za kujiuzulu au hatua nyingine kwa namna anavyoamini kuwa inafaa.
Msimamo wa CUF ulikuwa ni tofauti na ule wa Hamad ambaye mara kadhaa alishanukuliwa akisema kwamba hawezi kujiuzulu na kwamba, waliokuwa wakishinikiza suala hilo ni wasiopenda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
"Siwezi kujiuzulu kwa sababu kilichotokea ni mipango ya Mungu, hivi ningezuiaje upepo usitokee, ajai hii ni mipango ya Mungu, haiwezi kuzuiliwa na binadamu,” alisema waziri huyo.
Maiti tano zaopolewa
Wakati huohuo, Balozi Seif aliwaambia waandishi wa habari kwamba, maiti zaidi zimeopolewa na kufanya marehemu waliotokana na ajali hiyo kufikia 78.
Alisema miili iliyopatikana ilikimbizwa kuzikwa eneo la Kama nje kidogo ya Mji wa Zanzibar ambako kumetengwa kwa kuzikiwa maiti hizo.
Balozi Idd alisema kwamba, mpaka sasa jumla ya watu 146 wameokolewa wakiwa hai huku maiti zikifikia 78 ambazo ni pamoja na wanaume, wanawake na watoto.
Kuhusu juhudi za uokoaji, alisema meli hiyo ilikuwa na raia wa kigeni 17 na waliookolewa wakiwa hai ni 15 na mmoja ambaye ni raia wa Uholanzi alipatikana akiwa amefariki na mwingine mmoja hakupatikana hadi jana.
Wageni walinusurika kufa katika ajali hiyo wanatoka Ubelgiji, Marekani, Ujerumani, Uholanzi na Israel kwamba, Serikali iliwahudumia na tayari wameondoka kurudi kwao.
Balozi Idd aliongeza kuwa, hadi jana, kati ya majeruhi 138 waliopelekwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja iliyopo mjini Zanzibar kwa uchunguzi walikwisharuhusiwa kwenda kwao baada ya kupata matibabu.
Aliwataka wananchi popote watakapoona maiti wapeleke taarifa Jeshi la Polisi, wakuu wa wilaya, mikoa na masheha ili taratibu za kuichukua na kuihifadhi miili hiyo ziweze kuchukuliwa.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema miongoni mwa maiti hao mmoja imetambuliwa kuwa ni Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ, Kikosi cha Bendi Zanzibar aliyetambuliwa kwa jina la Suleiman Pandu Jape.
Meneja wa MV Skagit
Makachero wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, wamemsafirisha kwenda Zanzibar
Meneja wa Meli ya Skagit, Omari Hassan Mnkonje (50) ili kuunganishwa na watuhumiwa wengine wanaohojiwa na Polisi visiwani humo kuhusiana na meli hiyo.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi Zanzibar ACP, Yusuf Ilembo, alisema meneja huyo wa ambaye ofisi zake zipo Jijini Dar es Salaam ameunganishwa na watuhumiwa wengine katika kesi hiyo.
Katika hatua nyingine, Kamanda Ilembo amesema kuwa watuhumiwa watatu kati ya sita waliokuwa wakihojiwa kuhusiana na tukio hili wameachiwa baada ya kuonekana kuwa hawahusiki katika tukio hilo.
Habari na Salma Said na Talib Ussi, Zanzibar
Taarifa za nyongeza na Mohammed Mhina, Polisi Zanzibar na Joseph Zablon, Dar es Salaam.
Chanzo - http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment