Thursday, August 30, 2012

Aina mbili za watu wanaoweza kukukatisha tamaa

 
 
KWA sehemu kubwa, maisha ya mwanadamu yanategemea sana ushirikiano wa watu wenzake. Watalaamu wanasema mafanikio na kutofanikiwa ni watu.
Huwezi kusema umefanikiwa kisiwani kusikokuwa na watu ambao watakuwa sehemu ya mafanikio yako. Mtu yeyote hataonekana ameendelea kwa kuwa na viwanda vingi msituni wanakoishi wanyama wasiofahamu umuhimu wa nyama ya kusindika.
Aidha, kipimo cha kutofanikiwa hakitokani na maisha ya upweke bali ya kujilinganisha na watu wengine wanaozunguka maisha yako ya kila siku. Tajiri wa kijijini ni yule anayemiliki Bajaj ambazo wengine kwenye eneo analoishi hawana.
Ni ukweli ulio wazi kwamba utajiri wa mtu wa shamba wanakoishi maskini wengi hauwezi kuwanyima usingizi matajiri wa mjini wanaotembelea magari na kuishi kwenye nyumba za kifahari. Maana yangu hapa ni kwamba maisha ni watu.
Siku zote kwenye maisha yangu ninapokutana na binadamu wenzangu huwafikiria katika sehemu mbili. Kwanza kukwama kokote katika maisha kutatokana nao, lakini pili, ni kufanikiwa kwangu sehemu ya ninachokitarajia kutoka kwao.
Ufahamu huu umenisadia sana. Kila mara niwapo na rafiki zangu huwatazama katika sura hizo mbili kwamba nifanikiwe au nisifanikiwe kwa ajili yao.
Nimetafakari na kuamini kuwa somo la aina mbili za watu wanaoweza kukukatisha tamaa kwenye maisha yako linaweza kukusaidia, msomaji wangu, kufikia ujuzi wa elimu ya jinsi ya kufahamu namna binadamu wenzako wanavyoweza kukuletea mafanikio au kutofanikiwa.
Bila shaka katika maisha yako umekutana na watu ambao walikukataza usifanye jambo fulani ambalo wewe uliamini kabisa lingekusaidia kufikia mafanikio uliyokusudia kwenye maisha yako.
Sikia kauli hii: “Jambo unalotaka kufanya haliwezi kufanikiwa, unajisumbua bure.” Yawezekana ulishaambiwa hivi na ukaogopa, ukasita, ukakata tamaa ya kuanzisha biashara kwa sababu rafiki, wazazi au ndugu zako wamekuambia hutaweza kufanikiwa.
Naomba ujifunze kwamba, watu ambao ni hodari kwa kauli za aina hii ni wale wanaotoka katika makundi mawili hatari.
KWANZA ni wale wanaoogopa kujaribu kufanya jambo.
 
 PILI ni wale ambao hawapendi kukuona unafanikiwa kwenye maisha yako.
Mtu ambaye ni mwoga wa kujaribu, usitegemee hata siku moja atakumbia “fanya”. Anachojua yeye ni kueneza woga wake. “Bwana usiende kubeba zege utapata matatizo ya kiafya, usifanye hiki na kile kuna hili na lile,” hizo ni baadhi ya kauli atakazokuambia.
Hivyo, kuwa makini na watu waoga wa kujaribu, usiwape nafasi ya kukukatisha tamaa, hutafanikiwa kamwe!
Kundi la pili la kuwa nalo makini ni la wale ambao wanaogopa utafanikiwa. Watu ambao wanahofia uwezo wako utakufanya ufanikiwe na kuwashinda kwenye eneo hili na lile, watakupiga vita vya maneno ili kukukatisha tamaa, ubaki kama wao ambao hawakujaliwa uwezo ulio nao.
Puuza kauli za watu wasiopenda ufanikiwe, hata wakikuambia kuwa kusoma kwako hakutakusaidia waambie: “Kama ninyi mmesoma na hamkufanikiwa, ni ninyi lakini mimi mafanikio yangu ni elimu.”
Asante kwa kunisoma, tukutane tena wiki ijayo kwa somo lingine zuri zaidi.

No comments:

Post a Comment