Saturday, June 9, 2012

HIKI NDICHO ALICHOKISEMA MPIGANAJI ATHMANI HAMISI LEO KATIKA MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI


Mimi Athumani Hamisi
Awali ya yote, napenda kuwasalimia wote, wakubwa na vijana wenzangu
Hii itakuwa mara ya pili kuongea nanyi waandishi wenzangu, ndani ya miaka minne tokea nipate ajali Septemba 12, 2008 eneo la Kibiti Mkoani Pwani nikiwa na wenzangu Herry Makange ambaye kwa sasa ni marehemu na Anthony Siyame, tukiwa njiani kwenda Kilwa mkoani Lindi  kikazi. Mara ya kwanza niliongea nanyi 2010 baada ya kurejea kutoka Afrika kusini nilikopelekwa na Serikali kwa matibabu.
Shukrani zangu za awali, zimwendee Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete aliyenitembelea katika Hospitali ya Muhimbili nilikolazwa na kuagiza nilipelekwe nje kwa matibabu zaidi.
Katika ajali ile, nilivunjika shingo na ku-damage spinal cord iliyopelekea kupooza mwili wote kuanzia shingoni. Katika operesheni iliyofanywa na madaktari wa hospitali ya Mil Park, Afrika Kusini walilazimika kuunganisha shingo kwa nyuma.
Shukrani za pili ni kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kampuni  ninayofanyia kazi ya magazeti ya serikali, wachapishaji wa Daily News, Sunday news, Habari Leo Jumapili na Spoti leo, familia yangu iliyokuwa katika wakati mgumu wakati huo hadi sasa watanzania wote wuamini wa dini zote waliokuwa wakiombea Pamoja na marafiki zangu waliokuwa wakihangaika huku na kule kwa namna moja ama nyingine .
Niko mbele yenu leo kuwaomba mnifikishie ujumbe kwa jamii kwa maelezo yafuatayo:-
  1. Ofisi yangu ya TSN ilinipangia nyumba ninayokaa Sinza Vatican, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es salaam Mei 2010-2011 na mkataba ulikukwa kati ya mwenye nyumba na TSN ambao mimi sikuwahi kuuona hadi ninavyoongea na nyie leo.

  1. Mkataba uliisha tena Mei 2011, mwenye nyumba alikwenda TSN kuomba kusaini mkataba mpya. Badala yake aliandikiwa mkataba mpya wenye jina langu na kupewa aniletee mimi nisaini. Nilipomuuliza mkataba wa kwanza uliingia na nani na ni nani alisaini. Alisema ni TSN walisaini wakamwambia wana mgonjwa ambaye ni Staff wake atakuja kuishi pale akitokea Afrika Kusini alikokwenda kwa matibabu. Mwenye nyumba akasema walimwambia gharama za nyumba ni za TSN , sasa nashangaa leo wameandika jina lako na mkataba ni kati yangu na wewe.
  1. Nikamwambia kaka, mimi sikutarajia kufikia hapa kwani mwaka 1999 ilipangwa mimi nifikie katika nyumba ya kampuni Upanga kuepusha gharama na ukaribu wa huduma za kitabibu, mpaka masuala yangu yatakapothibitishwa na Daktrari kama hali yangu itaruhusu mimi kuweza kufanyakazi ama vinginevyo. Rudi ofisini  mkasaini kama mlivyofanya awali. Na umwambie kwa hali ya Athumani hawezi kusaini mkataba na mimi kulingana na hali yake. Isitoshe mi nilitiliana saini mkataba wa awali na TSN.
  1. Ukweli nilikataa kusaini zaidi ya mara tatu, mpaka Meneja Mwajiri siyo huyo wa sasa alipoingilia kati na kunithibitishia kuwa kampuni italipa nyumba mpaka uamuzi wa madaktari utakapotoka, saini mimi nitakulinda. Niliporejea nyumbani nikawekwa wino katika dole gumba wakaweka saini. Mpaka yalipojitokeza ya sasa.
  1. Ndugu waandishi wa habari, hali yangu japo imeimarika zaidi kuliko awali, leo nimekuja na jambo ambalo litahusisha jamii na nyie ndiye wahusika wakuu katika suala hili.
KIKUBWA ZAIDI LEO NI SHUKRANI NA OMBI
Ukweli ulio wazi, nashukuru  kwa Mungu na kujivunia kuwa TSN . nimelelewa na TSN kwa miaka sita sasa. Imenilea nikiwa mgonjwa kwa miaka mine, nikiwa bado niko ndani ya ajira jambo ambalo ni gumu sana sehemu nyingine.
Imelipa nyumba kwa miaka miwili na imesitisha kulipa kodi ya 2012-2013 kwa  barua ya Februari 3,2012 na kutoa maelezo kwenye barua kuwa imefikia hatua hiyo kutokana na kuwapa wafanyakazi wake asilimia 15 ya mishahara yao kulipa nyumba. Nyumba walionipangia ni ya vyumba viwili na kodi iliyolipwa kwenye mkataba wa mwaka jana ni Milioni 4.8
Nilipatwa na mshutuko kidogo, nafsi ikanishauri niite menejiment nyumbani tushauriane katika hili. Walikuja Machi 28, na wakanipa pole ya kampuni tokea nirudi 2010 Shs 50,000. Lakini mazungumzo hayakuisha kutokana na muda na kuahidi kurudi wiki inayofuata kwa mazungumzo zaidi. Nimepewa notisi na mwenye nyumba April 23,2010.
Nadhani kutokana na kubanwa na kazi, hawakupata nafasi ya kurudi tena kumalizia mazungumzo. Kwa mtazamo wa kifikira ni wazi msimamo ulibaki palepale. Barua ya kusitisha kulipa kodi haikuja kwangu tu bali pia mwenye nyumba alipata.
UFAFANUZI
Kabla ya kuruhusiwa kurejea nyumbani Tanzania, Netcare Rehabilitation Hospital, wanautaratibu mzuri sana. Kabla ya kuwa –discharged wanakuruhusu ukae nje ya hospital kwa miezi mitatu, kama una mke au mume na kama huna utatafutiwa nurse awe wa kike ama wa kiume mimi nilipata nurse. Baada ya hapo una hudhuria mazoezi na vipimo kadhaa kwa miezi mitatu. Ukifaulu kumaliza miezi mitatu wewe na mwangalizi wako hasa wewe mgonjwa bila kupata matatizo, hapo wanaku-discharge.
Nilipiga simu kwa Katibu Kiongozi Ikulu wakati huo, Philemon Luhanjo na kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii anahitajika nurse kuja kukaa nami nje ya hospital kwa miezi mitatu, je mtanisaidiaje? Kwa kweli jibu lao lilikuwa moja tu hatutatuma nurse kutoka huku, tafuta huko huko, fedha za kumlipa, nyumba ya kulala, chakula na usafiri, andika  budget itume haraka tutalipa na wasiliana na ubalozi waje kujua unakaa wapi  na fedha zitatumwa ubalozini watakuwa wanakuletea.
Nilipata nurse na miezi mitatu ilipokaribia kwisha nilifanya mawasiliano kujua kama kutatumwa mtu wa kunifuata, wakanijibu njoo naye huyo huyo watanzania waliofanikiwa kuangalia vyombo vya habari wengi walimuona kwani nilirudi Mei 28, 2010. Baada ya mwezi alimaliza mkataba name kutakiwa kutafuta nurse wa kukaa naye kwa saa 24 . akapatikana na akafundishwa na M-South Africa jinsi ya kukaa na mgonjwa wa Spinal Cord.
TSN, wakamlipa nurse wa South Africa Rand 12,500 alizokuwa anadai na palepale nikauliza vipi  kuhusu malipo ya nurse mpya ambaye ataachwa na mimi? Kwa sababu serikali imemaliza jukumu lake na waliniambia kwa kuwa wewe bado ni mwajiriwa wa TSN, jukumu lote sasa utakuwa chini yao na ndiyo mmepewa pia jukumu la kumlipa kama mlivyofanya leo. TSN walinijibu palepalekuwa suala la kumlipa nurse ni lako na familia yako ila nyumba tutalipa.

Vodacom walijitokeza kubeba gharama za tiketi nilipopata ajali kwenda Afrika Kusini na wasindikiaji wote, tiketi ya nurse niliyekuja naye. Pia wakalipa tiketi yangu na nurse Desemba 8,2010 kwenda na kurudi Afrika Kusini kwa ajili ya checkup.
Baada ya TSN kulipa nurse yule msouth afrika, nikawapigia Vodacom Foundation kuwa nurse amemaliza mkataba na ameshalipwa fedha naomba mumkatie tiketi. Hivyo  ilikuwa Juni 25 na kesho yake Juni 26 2010 jioni wakaja watu wawili kutoka Vodacom Foundation na mmoja kutoka TSN waliniambia wamekuja na vitu vitatu.
  1. Wakamshukuru  nurse kwa kazi nzuri , lakini wakamwambia , sisi ni kutoka  Vodacom. Vodacom Foundation inakuomba uendelee kumhudumia Athumani . Na Vodacom watakulipa mshahara lakina tunaomba upunguze kiwango.
  1. Yule nurse akakubali akapunguza nusu ya mshahara aliokuwa akilipwa na serikali. Wakamwambia sasa Vodacom Foundation inakata tiketi ya kwenda nyumbani Afrika kusini kuaga. Akaomba siku 15, mkataba  wa mdomo ukakubaliwa na yule nurse na mshahara wa kwanza ukawa Julai 2010 kuendelea na kazi chini ya Vodacom. Julai 2010 wakamlipa. Kilichoendela naomba nisiseme.
  1. Muda wa checkup ulifika Desemba 2010, nikaitaarifu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Wakakubali wakaandika barua kwa kugawa majukumu. Afya wakasema watalipa gharama  za matibabu, Vodacom tiketi za kwenda na kurudi na TSN waliagizwa kulipa allowance kwa mgonjwa na nurse. Tukasafiri Desemba 8,2010 na tukarudi Februari 28,2011. Malipo yaliyofanywa na TSN kidogo ni aibu naomba nisiseme.
  1. Hali hiyo ilinionyesha kuwa Vodacom Foundation walikuwa wanatambua uwepo wa yule nurse. Lakini hadi nurse anaondoka alilipwa mshahara mmoja tu na hata tiketi ya nurse kurudi Afrika Kusini Vodacom hawakulipa.
  1. Nililipa tiketi ya Business Class. Nikampa Rand 4,500 akakataa akachukua Rand 2,500 tu , akaniambia, Athumani nakuacha katika hali mbaya sana. Fuatilia haki zangu na zako, ukifanikiwa utaniambia na Account ya benki , First  bank nakuachia utaniwekea. Vodacom Foundation hawajawahi kupokea simu yangu na Mkurugenzi wake hajawahi kupokea simu yangu wala kuongea na mimi tokea nipate ajali.
  1. Suala lingine waliniuliza nichague kitu kimoja, kujengewa nyumba au kusomeshewa watoto. Mimi nilichagua kujengewa nyumba. Walichukua chaguo langu. Tukamaliza mazungumzo.
  1. Baada ya mwezi waliniambia suala lako limekubaliwa ila tumepata Mkurugenzi mpya, lakini usijali. Mpaka hapa ninavyoongea danadana ziliendelea mpaka ninavyoendelea kwenye nyumba, sijawahi tena kupata jibu kutoka Vodacom.  La mwisho nilijibiwa na mmoja wa watu wa Vodacom Foundation aliniabmia wewe uliingia mkataba na kampuni ya One Plass na si Vodacom Foundation.
SIKU YA LEO
Nimekuja leo kuutangazia umma hali ilivyo. Ukweli kwa sasa Account ya CRDB ilikuwa  maalumu kwa ajili ya kusomeshea watoto, imekauka ya Postal bank ambayo  ya mshahara haina kitu. Pesa ya mshahara inayoingia benki ni 450,000
Nawalipa nurse, msaidizi wake na mfanyakazi 370,000. Maisha ya ulemavu ni ghali sikutarajia . nina wanangu watatu, wa kwanza anamaliza darasa la saba mwaka huu, wa pili yuko la nne na wa mwisho yuko la pili.
Hawa wanasoma primary za kulipia wote hawa nawalipia 200,000 kila mmoja kwa term jumla 400,000 hizo shule zina term nne kwa mwaka. Gharama chakula, vifaa vya wanafunzi, gharama zao ndogondogo na za kifamilia Pamoja na chakula kwa mwezi , inakwenda kati ya 750,000 mpaka 900,000 kwa mwezi.
Nimekuwa ombaomba mpaka watu kadhaa siwalaumu, wamechoka hawapokei simu wala kujibu sms  . siyo siri ndugu wote wamekimbia waliobaki ni marafiki wa kweli wameniingiza katika familia zao. Hali yangu ni mbaya sana kiuchumi.
Sina uwezo wa kulipa nyumba kwa gharama zozote zile. Mimi Athumani Hamisi, naomba watanzania watakaoguswa wanisaidie. Kubwa nyumba na ushauri wa madaktari walinishauri nisiishi mbali na mazingira ya hospitali kulingana na hali yangu.
Makampuni , mashirika, wizara yoyote, shirika la nyumba la Taifa NHC, watu binafsi, serikali na Taasisi yoyote watakaoguswa na kilio changu nawaomba wanisaidie kwa njia yoyote . kwa walio tayari  naomba misaada ipitie katika account No 01J2027048800 ya CRDB na Account No 010-00090488 ya Postal Bank
Kwa wanaotumia mitandao ya simu, wanaweza kutumia M-pesa 0757 825 737, Tigopesa 0655 531 188 na Airtel Money 0784 531 118; M-Pesa 0767 298 888 ya Chris Mahundi na Airtel Money 0686 710 977 ya Ephraim Mafuru
Athumani Hamisi
0784 531 188 | 0655 531 188

No comments:

Post a Comment