Ndugu
Wananchi,
Kama ilivyo
ada naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma, kwa kutujaalia
uzima na kutuwezesha kumaliza nusu ya kwanza ya mwaka 2012 salama. Kwa kutumia
utaratibu wetu wa kuzungumza nanyi kila mwisho wa mwezi, leo napenda kuzungumzia
mambo mawili. Jambo la kwanza ni suala la usafirishaji haramu wa binadamu nchini
na la pili ni la mgomo wa madaktari.
Usafirishaji Haramu wa
Binadamu Nchini
Ndugu
Wananchi,
Bila ya shaka mtakuwa mmezisikia taarifa za
tukio la kushtusha na kuhuzunisha la kukutwa maiti 43 za watu
wasiojulikana, zilizotupwa katika kichaka kilichopo kijiji cha Chitego, Wilayani
Kongwa, Mkoa wa Dodoma tarehe 26 Juni, 2012. Pamoja na maiti hao,
walipatikana watu 84 wakiwa hai lakini wote wakiwa wamedhoofu na baadhi
yao wakiwa mahututi. Hatua za haraka zilichukuliwa kuwasafirisha watu hao hadi
Dodoma ambapo wale waliokuwa mahututi walifikishwa Hospitali Kuu ya Mkoa wa
Dodoma kwa matibabu na wengine walihifadhiwa katika Kituo cha Kati cha Polisi,
Dodoma. Maiti 22 zilipelekwa Dodoma na 21 zilipelekwa Morogoro
kuhifadhiwa.
Taarifa
zilizopatikana kutoka kwa wale walionusurika zimebainisha kuwa watu hao ni raia
wa Ethiopia ambao walikuwa safarini kwenda Malawi na baadaye Afrika ya Kusini
ambako wangetengenezewa utaratibu wa kwenda kuishi Marekani na Ulaya. Kwa
mujibu wa maelezo yao, safari yao ilianza miezi mitano iliyopita. Mwezi mmoja
waliutumia Ethiopia na miezi minne waliitumia Kenya kabla ya kuletwa Arusha
ambako walipakiwa kwenye lori na kuanza safari ya kuelekea Malawi lakini
ikaishia Chitego. Lori walilopanda lilikuwa limezibwa kabisa na hivyo
kusababisha vifo kwa kukosa hewa.
Tukio la
Chitego, Dodoma la wahamiaji haramu kukamatwa na wengine kukutwa wamekufa si la
kwanza kutokea hapa nchini. Kwa jumla, katika kipindi cha takriban miaka 10
sasa kumekuwepo na tatizo kubwa la wahamiaji haramu kuingia nchini. Kwa mfano,
kati ya mwaka 2005 na hivi sasa jumla ya wahamiaji
haramu 19,683 wamekamatwa. Karibu wote wameshaondoshwa nchini na hivi
sasa wapo karibu watu 1,500 tu magerezani wanaotumikia adhabu na kusubiri
kurejeshwa makwao. Wengi wa watu hao wanatoka Ethiopia na Somalia na baadhi
kutoka Pakistan na Bangladesh.
Wahamiaji haramu wamekuwa
wanaingia nchini kwa kupitia njia zisizo rasmi. Wapo wanaotumia nchi kavu hasa
kupitia mikoa ya Mara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga. Na, wapo wanaopitia
baharini kwa kutumia fukwe za Pemba, Unguja na za mikoa ya ukanda wa Pwani ya
Tanzania Bara yaani Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara.
Ndugu Wananchi,
Kwa
mujibu wa kauli zao, watu hao wamekuwa wanaeleza kuwa hawaji nchini kuhamia bali
wao ni wapita njia tu. Wanaelekea Afrika ya Kusini ambako wameahidiwa kuwa
watatengenezewa mipango ya kuhamia Marekani na Ulaya. Watu hao pia
wamethibitisha kuwepo kwa watu maalum wanaojihusisha na usafiri wao tangu nchi
watokako na zote wanazopitia mpaka kule waendako. Aidha, wamesema kuwa wao
wanawalipa watu hao ili wawasafirishe na hakika si kiwango kidogo. Kwa jumla ni
kwamba hili si suala la uhamiaji haramu bali ni la biashara haramu ya
kusafirisha binadamu.
Ndugu Wananchi,
Kufuatia
vyombo vyetu vya usalama kuwa makini na watu wengi kukamatwa ndipo wasafirishaji
walipobuni njia za kuwasafirisha kama mizigo. Makontena, malori yaliyofunikwa
nyuma na matenki ya mafuta na ya maji yamekuwa yanatumika kwa ajili
hiyo. Usafiri wa aina hiyo ndiyo uliosababisha vifo vilivyotokea Dodoma tarehe
26 Juni, 2012 na vya watu 21 vilivyotokea mwezi Desemba, 2011 Mkoani
Morogoro, na vile vya watu 12vilivyotokea katika matukio mawili ya Mkoa
wa Mbeya, mwezi Mei, 2012.
Ndugu Wananchi,
Tarehe
27 Juni, 2012 nilikutana na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini
kuzungumzia tukio la Chitego na suala zima la biashara hii haramu na hasa mbinu
mpya inayotumiwa na wasafarishaji. Nilitoa pongezi kwa vyombo vya dola kwa kazi
nzuri waifanyayo kudhibiti shughuli za biashara hii haramu hapa
nchini. Tulielewana kuwa waendelee kuimarisha udhibiti huo kwa lengo la
kukomesha kabisa biashara hii.
Niliagiza pia kwamba
kikundi kazi nilichokiunda mwaka 2006 kushughulikia ujambazi sasa kielekeze
sehemu ya nguvu zake kukabili tatizo hili. Aidha, kwa pamoja tulikubaliana kuwa
nchi yetu ishirikiane na wenzetu wa Ethiopia, Kenya, Malawi, Msumbiji na Afrika
ya Kusini kutambua mawakala na kuwabana kwa mujibu wa sheria. Tayari
nimeshaanza kufanya mawasiliano na baadhi ya Wakuu wa Nchi hizo kuhusu
ushirikiano huo. Nashukuru wote wameafiki nchi zetu zishirikiane kwa pamoja
kuvunja mtandao huu mchafu na kutokomeza biashara hii haramu na inayodhalilisha
utu wa mwanadamu.
Ndugu Wananchi,
Napenda
kuchukua nafasi hii kuwashukuru wenzetu, wakazi wa vijiji vya Chitego na Mkoka
kwa kazi nzuri walioifanya. Kwa kweli, wenzetu wameonesha uzalendo wa hali ya
juu kwa kutoa taarifa mapema juu ya jambo lenyewe, lakini pia wameonesha utu kwa
kuwajali wageni waliokumbwa na janga hili. Naushukuru pia uongozi wa Mkoa wa
Dodoma na Morogoro ikiwa ni pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwa
kulishughulikia tatizo hilo kwa umakini mkubwa. Nimefurahishwa sana na
ushirikiano ulioonyeshwa na vyombo na taasisi mbalimbali za Serikali katika
kushughulikia suala hili.
Mgomo
wa Madaktari
Ndugu
Wananchi,
Jambo la pili
ni kuhusu mgomo wa Madaktari unaoendelea nchini hivi sasa. Nilipozungumza na
Wazee wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa Diamond Jubilee tarehe 12 Machi, 2012,
kuhusu mgomo wa Madaktari uliokuwa unaendelea wakati ule pamoja na kuelezea
chimbuko la mgomo na hatua iliyokuwa imefikiwa, nilielezea mazungumzo yangu na
viongozi wa Chama cha Madakari wakiwemo pia viongozi wa Jumuiya ya
Madaktari. Nilitoa taarifa kuwa tumeelewana kuwa watasitisha mgomo na watarudi
kwenye meza ya majadiliano na Serikali. Siku ile pia nilielezea matumaini yangu
kuwa mgomo ule utakuwa wa mwisho katika nchi yetu. Bahati mbaya matumaini yangu
hayo hayakuwa na hivi sasa tunashuhudia tena wagonjwa wakiteseka, kuhangaika na
wengine kufa kwa sababu ya kukosa huduma wanazostahili kwa vile madaktari wao
wamegoma tena.
Ndugu Wananchi,
Kama walivyoniahidi,
madaktari waliacha kugoma na viongozi wao walirudi kwenye mazungumzo na
Serikali. Kama ilivyoagizwa na Mahakama Kuu, Kitengo cha Kazi tarehe 8 Machi,
2012, kwa mujibu wa Sheria ya Mahusiano Kazini, Namba 6 ya mwaka 2004. Chama
cha Madaktari na Serikali walifika katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi
(Commission for Mediation and Arbitration) kwa ajili ya majadiliano. Kwa pamoja
na kwa ridhaa yao wote, pande hizo mbili ziliiomba Tume hiyo iwape fursa ya
kuzungumza wao wenyewe na wakimaliza mazungumzo wataenda kusajili makubaliano
yao. Tume ikawakubalia. Ni vizuri ikakumbukwa kuwa siku ile ya tarehe 8 Machi,
2012 Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, ilitoa zuio la mgomo pamoja na kuagiza
kuwepo mazungumzo baina ya pande mbili.
Ndugu Wananchi,
Kati ya tarehe 10 Aprili,
2012 na tarehe 30 Mei, 2012, vilifanyika vikao sita vya majadiliano kati ya
Serikali na Chama cha Madaktari. Katika mazungumzo hayo hoja au madai 12 ya
madaktari yalizungumzwa. Mambo hayo ni haya yafuatayo:
1. Posho ya kuitwa kazini (on call allowance) iwe asilimia 10 ya
mshahara.
2. Posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi (Risk allowance)
iwe asilimia 30
ya mshahara.
3. Madaktari wapatiwe nyumba grade A au posho ya makazi ambayo
iwe asilimia 30
ya mshahara.
4. Posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu iwe asilimia
40ya mshahara.
5. Madaktari walipwe posho ya usafiri ya asilimia 10 ya mshahara
au wakopeshwe
magari.
6. Madaktari wanaoanza kazi walipwe mshahara wa shilingi
3,500,00/= kwa
mwezi.
7. Madaktari wapatiwe Green Card za Bima ya afya.
8. Hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya
Afya na
Ustawi wa Jamii.
9. Viongozi wa Kisiasa kulazimisha kupewa rufaa nje.
10. Madaktari waliofukuzwa warudishwe kazini.
11. Huduma za afya ziboreshwe nchini.
12. Posho ya uchunguzi wa maiti iongezwe.
Ndugu Wananchi,
Katika mambo
hayo 12 pande zote mbili zilifikia muafaka na kukubaliana wa pamoja kwa
mambo saba. La kwanza, ni kuhusu usafiri wa kwenda na kurudi
kazini. Serikali ilieleza kuwa upo utaratibu kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi
wa Serikali Na. 3 wa mwaka 2011 wa kuwakopesha wafanyakazi wa Serikali fedha za
kununulia magari au pikipiki, samani na matengenezo ya magari. Ilikubaliwa kuwa
madaktari waitumie fursa hiyo.
Jambo la
pili, ni kuhusu madaktari kupatiwa Green Card za Bima ya Afya. Jambo hili
lilikubaliwa na Serikali na Wizara ya Afya imekwishachukua hatua za utekelezaji
wake.
Jambo la
tatu, ni kuhusu hatua za kinidhamu kuchukuliwa dhidi ya Watendaji Wakuu wa
Wizara ya Afya. Kwa pamoja walikubaliana kuwa suala hilo liko nje ya mamlaka ya
Kamati yao ya pamoja, waziachie mamlaka husika za uteuzi. Uongozi wa juu wa
Wizara umebadilishwa na sasa kuna uongozi mpya. Lakini, jambo la kustaajanisha
hata Waziri mpya wa Afya alipowataka waonane kuzungumzia hoja walikataa
kumuona. Kwanza walisema hawaoni sababu kwa vile wameyazungumza na Kamati yake
kwa miezi mitatu bila ya mafanikio
Jambo la
nne walilokubaliana ni kuhusu viongozi kulazimisha kupewa rufaa ya kutibiwa
nje. Walikubaliana mambo mawili. Kwanza, kwamba maelekezo ya Waziri
Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda kuwa madaktari wazingatie maadili ya kazi zao na
kukataa kutoa rufaa kwa mtu asiyestahili awe kiongozi au asiwe
kiongozi. Pili, walikubaliana kuwa hospitali zilizopo ziboreshwe ili
viongozi watibiwe hapa nchini. Ukweli ni kwamba kufanya hivyo ndiyo sera ya
Serikali. Nililieleza hili mwezi Desemba 30, 2005 katika hotuba yangu ya
kuzindua Bunge baada ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuongoza nchi
yetu.
Tumeiongeza sana bajeti
ya sekta ya afya kutoka shilingi bilioni 3002005/2006 hadi shilingi
trilioni 1.2 mwaka 2011/12 na imekuwa ya tatu baada ya miundombinu na
elimu. Tumeziimarisha hospitali za Mikoa kwa vifaa tiba na wataalamu wa
afya. Kazi inaendelea katika hospitali za Wilaya. Tumewekeza katika Hospitali
ya Muhimbili. Hospitali hiyo ilivyo leo sivyo ilivyokuwa miaka sita nyuma. Na
kazi inaendelea hasa katika maeneo ambayo tunapeleka wagonjwa nje. Matunda yake
yanaanza kuonekana kwa upande wa figo, moyo, kinywa na mipango inaendelea kwa
upande wa ubongo na mishipa ya fahamu. Tunaendelea kuimarisha mafunzo
ya madaktari na madaktari bingwa, yote kwa nia hiyo hiyo. Hivi sasa Chuo Kikuu
cha Sayansi ya Tiba,Muhimbili kinachukua wanafunzi wengi zaidi ya ilivyokuwa
siku za nyuma na makazi mapya ya chuo yanaendelea kuandaliwa ili kuchukua
wanafunzi wengi zaid. Mwaka 2005 tulikuwa na madaktari bingwa 46 mwaka
huu tunao 520.
Ndugu
Wananchi,
Jambo la
tano ambalo pande zote mbili zilikubaliana ni kuhusu madaktari
waliofukuzwa. Hawa ni wale Interns waliokuwa wamerudishwa Wizarani
kutoka Muhimbili na kupangiwa hospitali za Temeke, Ilala, Mwananyamala na
Lugalo. Hili ni jambo ambalo lilikuwa limemalizika kitambo na wote walikuwa
wamerudi Muhimbili.
Jambo la
sita ni kuhusu mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na madaktari kuhusu
kuboresha huduma ya afya. Mapendekezo hayo yalihusu kutathmini sera na mpango
wa afya ya msingi, bajeti ya afya kuwa asilimia 15 ya bajeti ya Serikali,
kuwepo na utaratibu mzuri wa kuajiri madaktari na kuboresha viwango vya ubora wa
madaktari na kadhalika. Serikali imeyaafiki mapendekezo hayo na yatafanyiwa
kazi.
Jambo la
saba, ambalo pande zote walilokubaliana ni kuhusu kuongeza posho ya
uchunguzi wa maiti. Hili ni jambo jipya halikuwepo mwazoni. Hata hivyo,
Serikali imelikubali na posho hiyo imeongezwa kutoka shilingi 10,000/= hadi
kufikia shilingi 100,000/= kwa daktari na shilingi 50,000/= kwa
wasaidizi wake.
Ndugu Wananchi,
Kuna
masuala matatu ambayo yamekuwa na muafaka kwa kiasi fulani na
kutoafikiana kwa baadhi ya mambo. La kwanza ni suala la kufanya kazi
katika mazingira hatarishi. Serikali imekubali hoja ya kuchukua hatua ya
kuwalinda madaktari wanaofanya kazi katika mazingira hatarishi. Serikali
iliwaeleza kuwa watumishi wa kada zote za afya watapatiwa chanjo dhidi ya
maambukizi ya Hepatitis B na fedha zimetengwa katika bajeti ya
2012/13.
Aidha, Serikali imeeleza
dhamira ya kurudisha posho ya mazingira hatarishi kwa watumishi wa umma
wanaostahili. Utekelezaji wake utafanyika baada ya uchambuzi wa kina wa
kubainisha mazingira hatarishi ni yepi, viwango stahiki viwe vipi na nani hasa
wahusike. Madaktari wamekataa hili la kufanya uchambuzi, wanataka kiwango kiwe
kama wanavyotaka wao, yaani asilimia 30 ya mshahara na kianze mara
moja.
Jambo la pili
ambalo wamekubaliana nusu nusu ni kuhusu nyumba za kuishi. Serikali imekiri
wajibu wake wa kuwapatia madakari nyumba za kuishi. Aidha, imeeleza mpango
ulioanza wa kujenga nyumba 700 za madaktari kote nchini na kwamba hivi
sasa ujenzi wa nyumba 90 unaendelea,50 katika mkoa wa Mtwara
na 40 katika mkoa wa Rukwa.
Kwa maeneo ambayo
madaktari wanalipwa posho ya pango Serikali imesema waajiri wataendelea kufanya
hivyo kwa mujibu wa taratibu zilizopo kwa watumishi wa umma wenye stahili ya
kupewa nyumba. Jambo hilo limekataliwa na Madakari na kutaka lazima
walipwe asilimia 30 ya mshahara kama posho ya nyumba. Serikali kwa
upande wake imeona vigumu kufanya hivyo na kuwasihi wakubali wanayotendewa
wafanyakazi wengine wote wa umma.
Jambo
lingine ambalo lilikuwa na makubaliano ya nusu nusu ni kuhusu posho ya
kufanya kazi katika mazingira magumu. Pande zote mbili ziliafikiana kuwa yapo
baadhi ya maeneo nchini yanayo mazingira magumu kwa watumishi wa umma hivyo
hatua zichukuliwe kuwasaidia watumishi hao. Serikali imekubali wajibu wa kuweka
utaratibu wa kuboresha maisha ya watumishi katika maeneo hayo. Kwa ajili hiyo,
Serikali itatoa mwongozo kwa mamlaka za ajira kuhusu namna ya kuwasaidia
watumishi hao kupunguza makali ya maisha katika kila eneo badala ya kutegemea
posho peke yake.
Kuhusu posho, Serikali
imeeleza kuafiki kuwepo posho ya aina hiyo ila itatekelezwa baada ya kufanya
uchambuzi wa kuainisha mazingira husika, kutambua watumishi waliopo na gharama
zake.
Madaktari
hawajakubali kusubiri zoezi la uchambuzi lifanyike, wanataka Serikali ilipe
posho hiyo sasa. Tofauti hapa si posho hiyo kuwepo, bali ni rai ya Serikali ya
kubaini maeneo yenyewe na kupanga aina ya hatua na viwango vya posho kulingana
na mazingira halisi ya maeneo. Madaktari hawaoni haja ya kufanya
hayo.
Ndugu
Wananchi,
Mambo mawili
hayakuwa na muafaka kabisa kati ya pande zetu mbili. Jambo la kwanza ni posho
ya kuitwa kazini (on call allowance). Kwanza sina budi kueleza kuwa Serikali
imekubali kuongeza posho hiyo. Tangu Februari, 2012 posho iliongezwa
kutoka shilingi 10,000/= hadi shilingi25,000/= kwa daktari bingwa
(Specialist), shilingi 20,000/= kwa dakari mwenye usajili wa kudumu
(Registrars) na shilingi 15,000/= kwa madaktari waliohitimu ambao wapo
katika kipindi cha mafunzo kazini (Interns). Viwango hivyo vya posho vinatumika
hivi sasa.
Madaktari kwa upande
wao hawakukubali uamuzi huo wa Serikali na kusisitiza walipwe asilimia
10 ya mshahara. Ugumu wa kukubali pendekezo la madakari ni kuwa sharti la
malipo haya ni mtu kuitwa kazini. Ukitaka ilipwe kiwango cha mshahara ina maana
kuwa hata kama daktari hakupangwa kuitwa au alipangwa na hakutokea aendelee
kulipwa. Hili haliwezi kuwa sahihi kufanya. Linaweza kuwafanya baadhi ya
madaktari kutokutimiza wajibu wao kwa vile wana hakika mwisho wa mwezi malipo
yako pale pale.
Ndugu
Wananchi,
Jambo la pili ambalo muafaka haukufikiwa baina ya Serikali na madaktari ni kuhusu mshahara wa kuanzia kazi wa daktari. Madaktari wanataka uwe shilingi 3,500,000/= wakati Serikali inasema kiasi hicho hatukiwezi. Serikali imeeleza utayari wake wa kuongeza mshahara kwa kati ya asilimia 15 mpaka 20 kama ambavyo itafanya kwa watumishi wote wa umma katika mwaka huu wa fedha. Kwa kiwango cha sasa cha mshahara wao, daktari ataanzia kati ya shilingi 1,100,000/= na 1,200,000/= kutegemea kiwango kipi hatimaye kitaamuliwa. Madaktari wamekataa katakata na wameng’ang’ania shilingi 3,500,000/=.
Ndugu Wananchi,
Huo ndiyo mlolongo wa
mambo yaliyozungumzwa na pande zote mbili na matokeo ya mazungumzo
yenyewe. Katika kikao cha sita kilichofanyika tarehe 30 Mei, 2012, upande wa
Chama cha Madaktari ulisema kuwa kwa vile hoja ya nyongeza ya mshahara haina
mabadiliko hawakuona haja ya kuendelea na majadiliano mpaka watakapowasiliana na
wenzao. Waliahidi kutoa taarifa ndani ya wiki mbili. Tarehe 12 Juni, 2012, Rais
wa MAT aliandika barua kwa Katibu Mkuu Utumishi ambaye ndiye kiongozi wa
majadiliano kwa upande wa Serikali, kuwa Madaktari wameikataa taarifa na
ufafanuzi waliopewa kutoka Serikalini kwa ujumla wake.
Ndugu Wananchi,
Baada ya majibu yale ya
madaktari, tarehe 19 Juni, 2012, Serikali na Madaktari walikwenda kwa Msuluhishi
(CMA) kutoa taarifa kuwa mgogoro umekosa usuluhishi kama sheria inavyotaka. Kwa
pamoja pande zote mbili zilikubaliana suala hilo lifikishwe Mahakama Kuu Kitengo
cha Kazi. Wakati pande zote zinasuburi mgogoro huu kufikishwa ngazi hiyo ya
juu, upande wa Madaktari ukatangaza kuwepo kwa mgomo kuanzia saa sita ya usiku
tarehe 23 Juni, 2012. Hatua hiyo haikustahili kwani suala lenyewe halijafika
mwisho wa kushughulikiwa kwa mujibu wa Sheria za Mahusiano ya Kazi
nchini.
Ndugu Wananchi,
Tarehe 22 Juni, 2012,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali akaenda Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi kulifikisha
suala la tishio la mgomo na kuomba zuio la muda kufanywa. Mahakama Kuu
ilikubali ombi hilo na kuagiza kuwa mgomo usitishwe. Juhudi za kumtafuta Rais
wa MAT, Dkt. Namala Mkopi na viongozi wengine wa MAT hazikufanikiwa, Ofisi ya
MAT ilikuwa imefungwa na simu zote za viongozi wa MAT zilikuwa
zimezimwa. Hatimaye tarehe 25 Juni, 2012, alipatikana na kupewa amri hiyo ya
Mahakama. Tarehe 26 Juni, 2012, Dkt. Mkopi alifika Mahakamani ambapo alikana
kuwa yeye hahusiki na kuitisha huo mgomo lakini hakumtaja aliyehusika. Pamoja
na rai hiyo, Jaji alimuamuru Rais wa MAT akawatangazie wanachama wake kusitisha
mgomo. Dkt. Namala Mkopi hajafanya hivyo hadi leo na mgomo umekuwa unaendelea
kinyume cha Sheria.
Ndugu Wananchi,
Wagonjwa wanateseka na
wengine kupoteza maisha kwa mgomo huu usiokuwa halali kisheria ambao pia
haustahili kuwepo hata kwa mujibu wa maadili ya udaktari. Viongozi wa MAT na
wenzao wanawaingiza Madaktari katika mgogoro na Mahakama na waajiri wao
isivyostahili. Ni vyema viongozi wa Madaktari na madaktari wakatambua kuwa
wanashiriki katika mgomo usiokuwa halali ambao pia kiongozi wao mkuu amekana
Mahakamani kuwa hahusiki nao. Madaktari lazima watambue pia kwamba ajira zao
wanaziweka hatarini. Mfanyakazi ana kinga ya kutofukuzwa kazi na mwajiri kwa
kushiriki mgomo unaokubalika kisheria. Huu siyo. Watapoteza ajira, hawana pa
kukimbilia, hawana cha kiwalinda. Kwa madaktari interns, wanahatarisha maisha
yao kwani hawatapata cheti cha kudumu wakishiriki mgomo usiokuwa
halali. Lazima watafakari sana kwa hayo wafanyayo.
Ndugu Wananchi,
Napenda
kurudia maneno niliyoyasema tarehe 12 Machi, 2012, kuwa kuboresha mishahara na
maslahi ya wafanyakazi ni Sera ya Serikali yetu kwa maelekezo ya Ilani ya Chama
Tawala (CCM). Tumeitekeleza kwa vitendo sera hiyo, hata hivyo ni ukweli ulio
wazi kuwa nia yangu njema tu pekee haitoshi, lazima uwezo wa kufanya hivyo
uwepo. Kwa kulingana na uwezo uliopo, tumeendelea kuboresha mishahara na
maslahi ya wafanyakazi hatua kwa hatua tangu tuingie madarakani. Tumefanya
hivyo kwa jumla kwa wafanyakazi wote na kwa kada mbalimbali za watumishi wa
umma.
Miongoni mwa wafanyakazi
wa umma walionufaika na hatua hizo za Serikali ni madaktari na watumishi wa kada
nyingine za huduma ya afya. Tena nadiriki kusema madaktari tumewapa upendeleo
mkubwa kuliko watumishi wengine wa umma. Upendeleo upo kwenye mafunzo ambapo
wanafunzi wa udaktari wanagharimiwa na Serikali kwa asilimia mia moja wakati
wanafunzi wenzao wa taaluma nyingine hawako hivyo.
Ndugu Wananchi,
Mwaka 2004/2005, mshahara
wa kuanzia wa daktari ulikuwa shilingi178,700/=, mwaka 2005/ 2006
tuliupandisha na kuwa shilingi 403,120/=.Tuliendelea kuupandisha mwaka
hadi mwaka mpaka kufikia shilingi957,700/= wanazolipwa sasa. Kiasi hicho
ni mara mbili ya mishahara ya watumishi wa taaluma nyingine wenye shahada ya
kwanza wanaoanza kazi ambao kwa wastani hupata
shilingi 446,100/=.
Tunafanya hivyo kwa
kutambua na kuthamini nafasi maalum ya madaktari katika jamii na ukweli kwamba
bado tunayo safari ndefu ya kuziba pengo la madaktari nchini. Lakini inaonekana
juhudi zetu zote hizo hazithaminiwi.
Ndugu
Wananchi,
Sina budi
kusisitiza kwamba tunapofanya hivyo tunaongozwa na uwezo tulio nao wa
kulipa. Kwa sasa hatuwezi kuwaahidi kuwa tunao uwezo wa kuwalipa mshahara wa
kuanzia wa shilingi 3,500,000/= na posho zote zile. Tukifanya hivyo
malipo ya daktari anayeanza kazi yatakuwa shilingi7,700,000/=. Kwa
hakika kiasi hicho hatutakiweza. Si vyema kutoa ahadi hewa kwa watu
tunaowaheshimu na kuwathamini kama walivyo madaktari.
Kutokana na ukweli huo
basi kama daktari anayeona kuwa hawezi kufanya kazi Serikalini bila ya kulipwa
mshahara huo awe huru kuacha kazi na kwenda kwa muajiri anayeweza kumlipa kiasi
hicho. Nasi tutamtakia kila la heri. Hana sababu ya kugoma ili ashinikize
kulipwa mshahara huo. Asisumbuke, hatalipwa mshahara huo. Isitoshe, hana sababu
ya kuendelea kuwa na mgogoro na mwajiri ambaye hana uwezo wa kumlipa
anachokitaka. Huna sababu ya kumpa usumbufu mwajiri wa kukuandikia barua ya
kujieleza au kukuachisha kazi. Kwa nini upate usumbufu wa kupata barua hizo na
kuzijibu. Kwa nini upate usumbufu wa kuachishwa kazi na kutakiwa kuondoka kwenye
nyumba ya Serikali ndani ya saa 24. Jiepushe na yote hayo kwa kujiondoa
mwenyewe. Usipofanya hivyo, mwajiri anakuwa hana jinsi bali kukuondoa kazini
maana unakwenda kinyume na sheria za kazi na maadili ya kazi ya
udaktari.
Mamlaka za ajira
zimeanza kuchukua hatua hizo na wataendelea kufanya hivyo kwa wote wanaoendelea
kugoma. Najua baada ya hatua hizo kuchukuliwa kuna manun’guniko ya kuonewa.
Hivyo, mlitegemea mwajiri afanyeje? Ni bora kufanya hivyo ili ajue hana daktari
aweze kufanya utaratibu wa kuziba hilo pengo na huyo ajae awe na mahali pa
kuishi. Vinginevyo atakuwa anajidanganya kuwa anae daktari ambae hayupo kazini
na wala hataki kufanya kazi.
Ndugu
Wananchi,
Napenda kuwathibitishia
kwamba dhamira ya Serikali ya kuboresha maslahi ya watumishi wa umma
wakiwemo madaktari iko wazi. Tumekuwa tunafanya hivyo, na tutaendelea kufanya
hivyo kulingana na uwezo wa kibajeti. Ni vyema watumishi wa umma wakatambua
kuwa hatuwezi kutumia fedha zote au kiasi kikubwa mno cha pesa za umma kulipana
mishahara. Tukifanya hivyo, Serikali itashindwa kutoa huduma muhimu kwa
wananchi ambao ndiyo wengi na wanastahili kuhudumiwa. Hata hizo huduma za afya
tunazosema ni duni tuziboreshe, hatutaweza kuziboresha kama tutatumia sehemu
kubwa ya pesa za Serikali kuwalipa mishahara wafanyakazi.
Hivi sasa matumizi ya
mishahara ni asilimia 48 ya bajeti ya Serikali. Kiwango hicho ni kikubwa
mno. Uwiano mzuri ni kuwa na matumizi ya mishahara yasiyozidi asilimia
35 ya bajeti na asilimia 65 zitumike kugharimia huduma na shughuli
nyingine za maendeleo ya wananchi na taifa. Sisi tumezidi kwa asilimia
13. Hivyo, hatuna budi tukubali kujinyima kwa manufaa ya walio
wengi.
Suala
la Dkt. Steven Ulimboka
Ndugu
Wananchi,
Kabla ya kumaliza hotuba
yangu, napenda kuungana na Watanzania wenzangu wote kuelezea masikitiko yangu
makubwa na kuhuzunishwa kwangu na kitendo cha kinyama alichofanyiwa Dkt. Steven
Ulimboka usiku wa tarehe 26 Juni, 2012. Kitendo hicho ni kinyume kabisa na mila
na desturi zetu. Watanzania hatujayazoea mambo hayo. Nimeelekeza vyombo vyetu
vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane. Nimesema
kuwa ningependa ukweli huo ujulikane mapema ili tuondoe wingu baya la kutiliana
shaka na kulaumiana kunakoendelea hivi sasa.
Natambua kuwa Serikali
nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa shaka. Mimi nimeshangazwa sana na
hisia hizo kwani siioni sababu ya Serikali kufanya hivyo. Dkt. Ulimboka alikuwa
mmoja wa kiungo muhimu katika mazungumzo baina ya Serikali na Madkatari. Ni
kweli kwamba yeye si mtumishi wa Serikali, hivyo hakustahili kuwa sehemu ya
majadiliano haya. Kulikuwa na rai ya kutaka asiwepo, lakini nilisema wamuache
maadam Madaktari wanamuamini kuwa anaweza kuwasemea vizuri zaidi kuliko wao
wenyewe walioajiriwa na Serikali.
Ndugu
Wananchi,
Kama nilivyoeleza,
mazungumzo yalienda vizuri na mafanikio makubwa yamepatikana. Yapo maeneo
machache na hasa eneo la mshahara ambalo hatukuweza kukubaliana. Hapo
tulipofikia si pabaya na tulikubaliana sote kurudi kwenye mkondo wa Sheria
kusaidiwa. Kwa nini Serikali imdhuru Dkt. Ulimboka? Na, kuhusu mgomo, Mahakama
Kuu imekwishatoa amri ya kusitisha mgomo. Anayekaidi amri ya Mahakama ananunua
ugomvi na mhimili huo wa dola ambao wenyewe una mamlaka ya kumtia adabu mtu
huyo. Hivi baada ya kufika hapo Serikali iwe na ugomvi na Dkt. Steven Ulimboka
kwa sababu ipi na jambo lipi hata iamue kumdhuru? Kama kuna mtu wa Serikali
kafanya, itakuwa kwa sababu zake binafsi na siyo za Serikali au kwa kutumwa na
Serikali.
Ndugu Wananchi,
Kwa
niaba yangu na kwa niaba ya Serikali natoa mkono wa pole kwa Dkt. Steven
Ulimboka na kumuombea apone haraka ili aungane na familia yake na Watanzania
wenzake katika ujenzi wa taifa. Kwa namna ya pekee namshukuru na kumpongeza
Bwana Juma Mgaza, kwa moyo wake wa huruma na upendo na kwa hatua alizochukua za
kumsaidia Dkt. Ulimboka.
Naomba
kumaliza kwa kuwasihi madaktari kuacha mgomo na kurejea kazini. Watanzania
wenzenu wanateseka na kupoteza maisha. Muwe na moyo wa huruma na upendo na
msaada kwa wagonjwa kama kiapo chenu kinavyowataka.
Mungu Ibariki
Afrika!
Mungu Ibariki
Tanzania!
Asanteni kwa
Kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment