Wednesday, July 18, 2012

Kupima Ukimwi kwa mate kuanza mwakani




TUME ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids) imesema kipimo cha kupima ukimwi kwa kutumia mate kitaanza kutumika mwakani kwenye mahospitali.

Kifaa hicho kilichotengenezwa na wanasayansi wa nchini Marekani kimeelezwa kuwa na uwezo wa kutoa majibu sahihi kwa zaidi ya asilimia 90 kwa kati ya dakika 20 na 40 baada ya kupima.

Imeeleza kuwa kifaa hicho kinachofahamika kama OraQuick, kimebuniwa sio tu kwa ajili ya matumizi ya hospitalini bali pia nyumbani na kitaanza kupatikana katika maduka ya dawa nchini Marekani kuanzia Oktoba mwaka huu kabla ya kusambazwa nchi mbalimbali duniani.

Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa Tume hiyo, Beng’i Issa alisema kipimo hicho kitaanza kwanza kutumika kwenye hospitali na baada ya hapo wataangalia namna ya kuwaelimisha wananchi ili kiweze kutumika hadi kwenye ngazi ya jamii.

Mkurugenzi huyo alikuwa akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi msaada wa gari lililotolewa na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) kwenda kwa Umoja wa Mameya na Viongozi wa Manispaa na Majiji (AMICAALL).

“Ni new development (maendeleo mapya) ambayo imekuja na serikali imepjipanga kuanzia mwakani kitaanza kutumika,”alisema Issa.Alisema pia kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo kimeshuka kwa asilimia 25 wakati kwa vijana kimeshuka kwa asilimia moja.
Kwa mujibu wa Issa, watu wazima hasa walioko kwenye ndoa ndiyo walioathirika zaidi ikilinganishwa na vijana.

Alisema pia mwitikio wa watu kwenda kupima ukimwi nao umeongezeka kwa asilimia 40 ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo ilikuwa asilimia 10.“Tunawahamasisha wazazi kuongea na watoto wao na viongozi wa dini kutusaidia kuwarudisha watu kwenye maadili,”alisema.

Akizungumzia kuhusu msaada huo, Mwenyekiti wa Amicaall, Amani Mwamwindi alisema gari hilo litatumika kwa ajili ya kufuatilia shughuli mbalimbali za ukimwi katika manispaa na majiji.

Na Nora Damian

No comments:

Post a Comment