Wednesday, July 18, 2012

Mwanafunzi atoa msaada wa Sh30 milioni
MWANAFUNZI wa Shule ya Covel Reef High School ya jimbo la Miami nchini Marekani, Leah Singer (18), ametoa msaada wa zaidi ya Sh30 milioni kwa ajili ya kugharamia uchimbaji wa kisima kirefu cha kijiji cha Sekou Toure kata ya Ilongero jimbo la Singida Kaskazini.

Hayo yalisemwa juzi jioni na mbunge wa jimbo la Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, muda mfupi baada ya kumaliza kukagua maendeleo ya uchimbaji wa kisima hicho kitakachowakomboa wananchi 4,850 wa kijiji cha Sokoture ambao, wamekuwa wakipata adha kubwa kutokana na uhaba wa maji safi na salama.

Alisema mwanafunzi huyo kijana mdogo amefikia uamuzi huo wa kutoa msaada wa kuchimba kisima, baada ya kusoma taarifa ya hitaji la maji kwa wakazi wa kijiji hicho kwenye mtandao wake (Nyalandu).

"Leah baada ya kusoma habari hiyo, alitambua umuhimu wa hitaji hilo na mara moja alianza kuchangisha fedha na hatimaye amefanikiwa kutimiza lango lake na sasa tunashuhudia kisima hiki kirefu kinachimbwa," alifafanua Nyalandu ambaye pia ni naibu Waziri wa Maliasili na Utalii.

Katika hatua nyingine, mbunge huyo alitumia fursa hiyo kuwataka vijana nchini kuiga mfano wa Leah wa kuwa na moyo wa kujitolea.

Nyalandu alisema vijana wanapaswa kutambua kuwa kutoa misaada ni moyo na wala si kwa sababu mtu ni tajiri wa kiwango gani.

"Ukiwa na moyo wa kijitolea, unaweza ukafanya kazi halali ukapata fedha ambazo utazitumia kuwasaidia watu wenye mahitaji muhimu kama maji safi na salama. Pia unaweza kuchangisha kama alivyofanya Leah," alisema.

Akifafanua zaidi, alisema vijana wanao wajibu mkubwa wa kuanzia kuzisaidia familia zao kwa hali na mali na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake, Leah ambaye baadaye mwaka huu anatarajiwa kujiunga na Chuo Kikuu maarufu nchini Marekani cha Havard, alisema ataendelea na juhudi zake za kuchangisha fedha za kusaidia makundi ya watu wenye mahitaji muhimu yakiwemo ya maji safi na salama.
                                         Na Gasper Andrew, Ilongero

No comments:

Post a Comment