Friday, August 17, 2012

MKUU WA MKOA WA DSM AHIMIZA SENSA YA WATU NA MAKAZI, ATOA ONYO KWA WALE WANAOENDESHA VITENDO VYA VURUGU


Na. Aron Msigwa -MAELEZO.
Dar es salaam.
Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuanza kwa zoezi la Sensa ya watu na makazi nchini, mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadiki ametoa wito kwa wakazi wa mkoa huo kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa watakaoendesha zoezi hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es salaam amesema maandalizi ya ukamilishaji wa zoezi hilo yanaendelea vizuri na kuongeza kuwa Waziri mkuu Mizengo Pinda anatarajia kuzindua kampeni ya uhamasishaji wa watu kushiriki katika zoezi hilo kesho (17/8/2012) katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam.
Ametoa onyo na kuvitaka vikundi vya baadhi ya viongozi wa dini na wananchi wanaowahamasisha wananchi kutoshiriki katika zoezi hilo katika maeneo yao kuacha mara moja kwani zoezi hilo lipo kwa mujibu wa sheria namba 1 ya mwaka 2002.
"Natoa onyo kwa kikundi chochote kinachoendesha kampeni ya kuwahamasisha wananchi kutoshiriki kwenye zoezi la Sensa ya watu na makazi katika mkoa wa Dar es salaam kuacha mara moja kwani zoezi hilo lipo kwa mujibu wa sheria na yeyote atakayekaidi au kukwamisha zoezi hilo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake" amesema.
Amesema kuwa Zoezi la Sensa sio la mtu mmoja mmoja wala kikundi fulani bali ni suala la watanzania wote bila kujali dini, rangi wala kabila, hivyo watu wanaopinga zoezi hilo wanavunja sheria za nchi.
Naye mratibu wa zoezi la Sensa kwa mkoa wa Dar es salaam Bi. Magreth Stephen Mganda amesema mpaka sasa mkoa wa una jumla ya makarani na wasimamizi 18,993 watakaoshiriki zoezi la kuhesabu watu wakiwemo 90 wa akiba.
Amesema kati ya hao 644 wanatoka wilaya ya Kinondoni,365 wanatoka Ilala na 530 kutoka wilaya ya Temeke.
Katika hatua nyingine mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Bw. Saidi Meck Sadiki ametoa ufafanuzi wa vitendo vya vurugu,uharibifu na uporaji wa mali za wanachi katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es salaam hususan wilaya ya Temeke na Kinondoni.
Amesema kuwa vitendo hivyo vilivyotokea ni kinyume cha sheria na kutoa onyo kwa wale wote waliohusika kuvamia maeneo na kuchukua ardhi kwa nguvu pasipo kufuata utaratibu kuacha mara moja.
Amesema kuwa wale waliovamia maeneo hayo bila kufuata utaratibu waondoke wenyewe na kukubali kutii sheria bila shuruti kwa kuwa serikali haitamvumilia mtu yeyote anayevunja sheria.
"Wale wote waliovamia maeneo hayo katika mkoa wa Dar es salaam katika maeneo yote yenye vurugu waondoke wenyewe , watii sheria kwa sababu vitendo vya namna hii ni vya kiharifu na kamwe serikali haiwezi kuvivumilia" amesisitiza.
Ameongeza kuwa tayari mahakama imeshatoa mwongozo kuhusu maeneo hayo na kubainisha kuwa wote waliohusika na watakaoendelea kuvunja sheria katika maeneo hayo watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

No comments:

Post a Comment