Mkurugenzi wa makosa ya jinai nchini (DCI) Robert Manumba (mwenye miwani), akitoa taarifa hiyo |
Jeshi la polisi Tanzania limekamata watu watano jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Alberatus Barlow na bado linaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine.
Akiongea na waandishi wa habari jijini Mwanza Mkurugenzi wa makosa ya jinai nchini (DCI) Robert Manumba amewataja watu hao kuwa ni muganizi Michael (36) Mkazi wa Isamilo ambae alikiri kumuua kamanda kwa risasi.
Wengine ni Chacha Waitara Mwita (50), Magige Mwita Marwa, Bugazi Edward Kusota na Bhoke Mara Mwita(42). Watuhumiwa hawa walikamatwa baada ya kuwekewa mtego na kwa ushirikiano kati ya jeshi la polisi na wananchi.
Manumba alisema kikosi kazi cha upelelezi kilichokuwa chini yake kilijigawa kwenye makundi matatu, yaani kundi la ukamataji, mahojiano na kundi jingine la intelejensia ambapo walitumia njia ya kisayansi kwa kufuatia mitandao ya simu. Na kwamba jeshi hilo limefanikiwa kukamata bunduki iliyotumiwa kutekeleza mauaji hayo na simu aliyoporwa mwanamke aliyekuwa amesindikizwa na Kamanda Barlow na bado polisi inasaka radio call aliyokuwa nayo marehemu.
Watuhumiwa hao watano wanafikisha idadi ya watuhumiwa kumi wanaoshikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za mauaji hayo.
Marehemu kamanda Barlow aliuawa usiku wa Oktoba 12 kati ya saa saba na saa nane eneo la, Kitangiri, Kona ya Bwiru mkoani Mwanza baada ya kupigwa risasi na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi alipokuwa anamsindikiza mwalimu Dorothy Moses nyumbani kwake.
No comments:
Post a Comment