Mawakili
wa utetezi katika kesi ya mauaji ya Steven Kanumba (28) inayomkabili
msanii wa filamu nchini Elizabeth Michael (18) maarufu Lulu,
wamewasilisha Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam vielelezo
vya kuthibitisha kwamba mteja wao ana umri wa miaka 17.
Vielelezo
hivyo, viliwasilishwa jana mahakamani hapo kwa njia ya maandishi
kupitia kiapo na jopo la mawakili hao mbele ya Jaji Dk. Fauz Twaib
anayechunguza umri halali wa mshtakiwa huyo.
Katika
ushahidi uliowasilishwa, baba mzazi wa Lulu, Michael Kimemeta, ameapa
kwamba binti yake hadi anatuhumiwa kufanya tendo hilo la mauaji umri
wake ni miaka 17.
Kimemeta anadai kwamba, Lulu alizaliwa miaka 17 iliyopita akiwa mkoani Kilimanjaro.
“Wakati
anazaliwa binti yangu nilipata taarifa nikampa jina la Elizabeth
Michael wakati huo mama yake Lucresia Kalugila alikuwa tayari kampa jina
la Diana Michael” alisema na kufafanua:
“Baada
ya kumfahamisha napenda aitwe Elizabeth ililazimika kuongeza Diana
Elizabeth Michael Kimemeta, majina yote mawili ni yake.”
Alidai kuwa, Lulu alibatizwa Septemba 28, mwaka 1997 katika Kanisa Katoliki la Chang’ombe na ushahidi wa cheti cha ubatizo upo.
Kwa
upande wake, Kalugila ambaye ni mama mzazi wa Lulu, alidai kuwa
alijifungua mtoto huyo miaka 17 iliyopita katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili ya Jijini Dar es Salaam.
Upande
wa Jamhuri unaoongozwa na Wakili wa Serikali, Shadrack Kimario, utajibu
ushahidi huo Juni 20, mwaka huu na maombi hayo yatasikilizwa Juni 25
mwaka huu.
HABARI NA HELLEN MWANGO
CHANZO: NIPASHE
mungu amsaidie huyu mtoto jamani
ReplyDelete